Nakusalimu katika jina la Bwana wetu YESU Kristo aliye hai, ashukuriwe Mungu wa mbingu na ardhi kwa kutupa nafasi nyingine tena ya kulitafakari NENO Lake tukiwa tumekusanyika pamoja.

Tukiwa pamoja kanisani/hemani mwa Bwana kila mmoja wetu ana ujuzi na maarifa aliyomjalia Mungu kuwa nayo. Wapo wenye ujuzi na ustadi wa kutengeneza vitu mpaka ukavutiwa kuvitazama mara nyingi uwezavyo. Na wapo pia wenye ujuzi na ustadi wa darasani na kuzaliwa nao, hawa nao kila mmoja amempa nafasi yake ya kufanya vitu vizuri sana mpaka ukapenda.

Kwa nafasi ya kila mmoja mwenye ujuzi na maarifa kuhusu jambo fulani, ujuzi wao unatambuliwa sana na Mungu wapate kuutumia pale wanapohitajika kuujenga ufalme wa MUNGU.

Ujuzi wao wa kutengeneza vitu mbalimbali unaweza kutumiwa vizuri nyumbani mwa Bwana pasipo kutafuta watu wa nje. Kazi ikafanyika vizuri sana maana wanajua wanafanya kwa ajili ya Bwana wao aliye juu mbinguni.

Haijalishi watatumiwa na hema wanalosalia ama nje ya hema wanaosalia, ilimradi bado ni kazi ya Mungu. Watapaswa kuitikia kwenda kuifanya kwa moyo wote wa upendo.

Hili jambo tunaliona kwa mfalme Suleiman, anatafuta mafundi stadi wa kumjengea Bwana nyumba yake. Pamoja na kuwapata hawa mafundi watakaojenga nyumba ya Bwana, kwa kazi yao kubwa ya ustadi wa ufundi wao aliamua mwenyewe kuwalipa kiasi fulani.

REJEA: Na tazama, nitawapa watumishi wako, wachongaji wakatao miti, kori ishirini elfu za ngano iliyopondwa, na kori ishirini elfu za shayiri, na bathi ishirini elfu za mvinyo na bathi ishirini elfu za mafuta. 2 NYA. 2:10 SUV.

Sijakuambia uhakikishe unajua kwanza kiasi utakacholipwa ndipo ufanye kazi ya Bwana la hasha! Ninachokuonyesha hapa ni jinsi gani kazi ilikuwa kubwa mpaka mfalme Suleiman akaona mwenyewe awalipe kiasi hicho alichowaahidi kuwalipa.

Zipo kazi ambazo huhitaji malipo kutokana na kujitoa kwako, zipo pia kazi utafanya na utalipwa na mtumishi wa Mungu aliyewapa ile kazi kutokana na ukubwa wa kazi yenyewe uliyofanya.

Tunaona jambo lingine tena la msingi sana, ujuzi wako unalipa kabisa na unaweza ukaendesha maisha yako kimwili. Lisha ya ujuzi kulipa tunaona pia unatambulika vyema kwa watu wa MUNGU na jamii kwa ujumla.

REJEA: mwana wa mwanamke wa binti za Dani, na babaye alikuwa mtu wa Tiro, ajuaye sana kazi ya dhahabu, na ya fedha, ya shaba, ya chuma, ya mawe, na ya mti, ya urujuani, ya samawi, na ya kitani safi, na ya nyekundu; tena mstadi wa kuchora machoro yo yote, na wa kufikiri fikira yo yote; apate kuagiziwa kazi pamoja na watu wako wastadi, tena na wastadi wa bwana wangu Daudi baba yako. Basi sasa hiyo ngano na shayiri, mafuta na mvinyo, aliyonena bwana wangu, na wapelekewe watumishi wake; nasi tutakata miti katika Lebanoni, kadiri utakavyohitaji; na kukuletea tukiieleza baharini mpaka Yafa; nawe utaichukua Yerusalemu. 2 NYA. 2:14‭-‬16 SUV.

Usikumbatie ujuzi wako, usifiche kile unaweza kukifanya kwa uaminifu kwa wengine, usijifiche na usikatae pale unapohitajika kutenda kazi kanisani kwako au kanisa lingine jirani ambalo wewe husali pale.

Kujitoa kwako kunakupa nafasi nzuri zaidi ya kumtumikia Mungu wako kupitia nafasi yako ya ujuzi ulionao. Huenda huwezi kushika maiki ukapaza sauti ukawahuburia wengine, unaweza kutoa ujuzi na maarifa yako ukamzalia Bwana matunda mema sawasawa na aliyesimama kuhubiri/kufundisha NENO LA MUNGU.

Wapo watumishi wa MUNGU wana maono makubwa ya kuwaleta watu wengi kwa Kristo, kama ilivyokuwa kwa mfalme Suleiman alikuwa na maono makubwa ya kumjengea Bwana nyumba kubwa. Maana yalikuwa ni maono yaliyoishi babaye Daudi, lakini Mungu akamzuia mfalme Daudi asijenge nyumba yake kutokana kumwaga damu nyingi. Na badala yake alimwahidi mwanaye Suleiman ndiye atakayemjengea nyumba yake.

REJEA: Nayo nyumba nitakayoijenga ni kubwa; kwa sababu Mungu wetu ndiye mkuu juu ya miungu yote. 2 NYA. 2:5 SUV.

Ungane na watumishi wa MUNGU kupitia ujuzi wako, kutimiza maono yao ya kumtumikia Mungu kwa kuitenda kazi yao waliyochaguliwa waitende kwa kiwango kikubwa . Kushirikiana nao utakuwa umekuwa miongoni mwa watenda kazi katika kuujenga ufalme wa Mungu hapa duniani.

Kuna kitu umekipata baada ya kusoma ujumbe huu, kifanyie kazi kile ulichokipokea. Ili kiwe baraka hemani mwa Bwana.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu
+255759808081.