Usishtuke, ni kweli kabisa tunapaswa kulijua hili, maana wengi wamefunga na hali zao za kiroho zimekuwa mbaya zaidi.
Kufunga kwetu kumejaa maswali mengi sana, kufunga kwetu nyuma yake kumeacha alama za mishangao mingi.
Mtu anafunga usiku na mchana Mungu amsaidie kupata kazi nzuri, katika kutafuta kazi anakutana na boss anamtaka kimapenzi. Anaruhusu kulala naye kimapenzi na mkuu wa ofisi ile aliyoenda kuomba kazi.
Mtu anachukua maombi ya kufunga, ili Mungu ampe mume/mke mwema, na wakati huo tayari ana mwanaume/mwanamke analala naye kimapenzi.
Siku hajafanya naye uasherati, ni siku anasema anaingia kwenye maombi ya kufunga. Hapo ndio amepumzika uchafu wake, baada ya kumaliza maombi yake anarudi tena kwenye uchafu wake ule ule.
Mtu anachukua maombi ya kufunga ili apate mtoto, baada ya kukaa kwenye ndoa muda mrefu bila mtoto. Huku upande wa pili anahaigaika na waganga wa kienyeji waweze kumsaidia kupata mtoto.
Mtu wa namna hii anakuwa wa kwanza kulalamika Mungu hamjibu maombi yake, amesahau mambo yanayoyafanya hayampendezi kabisa Mungu. Amesahau au hajui kuwa Mungu sio wa michanganyo.
Mwingine anafunga sana, ili aonekane na yeye amefunga ila funga yake haina utukufu mbele za Mungu, bali ni ya majivuno mbele za watu kutaka sifa.
Rejea: Je! Kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na BWANA? Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira? ISA. 58:5-6 SUV.
Nakusihi sana, ikiwa unafunga funga bila kuelewa vizuri utaratibu unavyoenda, usifunge kabisa, sio nakufundisha kuishi maisha ya wokovu bila kufunga. Ukisoma vizuri hayo maandiko matakatifu niliyokuwekea hapo juu, utaona mstari wa mwisho ukitoa maelekezo namna ya kuwa na saumu njema mbele za Mungu.
Tengeneza kwanza na Mungu wako, usikimbilie kufunga huku una mambo ambayo hujaamua kuyaacha na haupo tayari kuyaacha. Yaache kwanza hayo yasiyompendeza Mungu, ndipo uingie kwenye maombi.
Kiongozi wa mambo yote ni Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081