Bwana Yesu asifiwe mwana wa Mungu, bila shaka umeamka salama na unaendelea kumtukuza Mungu kwa wema wake mkuu kwako. Kama umeamka unaumwa Mungu akakuponye na kurejeshea afya yako katika jina la Yesu Kristo.

Kumekuwa na tabia moja ya ajabu sana kwa vijana walio wengi leo, kijana yupo ndani ya mahusiano ya uchumba/urafiki na dada/kaka fulani. Huyu kaka/dada anashindwa kuwa mwaminifu kwa mwenzake na wakati mwingine sio ameshindwa kuwa mwaminifu bali ni tabia yake chafu aliyonayo.

Siku isiyojulikana huyu kaka/dada anamkuta mchumba/rafiki yake huyu wenye mipango ya kuishi pamoja kama mume na mke siku za hivi karibuni. Anamkuta yupo na kaka/dada mwingine kabisa ambaye baadhi ya marafiki wanamjua kama watu na mpenzi wake.

Wewe unayejua una mchumba mwaminifu na anayekupenda, leo unamkuta yupo na mwingine tena wanafanya vitendo viovu. Badala ya kumshukuru Mungu amekuonyesha mapema mtu uliyekuwa unatarajia kuishi naye kama mwenzi wako wa maisha, sio mtu mwaminifu kama ulivyokuwa unafikiria na kumwona wewe. Badala yake unaanza kupigana/kugombana na huyo uliyemkuta na mchumba wako.

Nikueleze tu ukweli ukiona unagombana na wanaume/wanawake unaowakuta wapo na huyo mchumba wako, tena wakati mwingine unawafuma kabisa katika mazingira ya kufanya uasherati. Ujue kabisa haupo makini na maisha yako yajayo, na uhusiano wako na Mungu una mashaka makubwa sana.

Kijana mcha Mungu katika roho na kweli hawezi kuwa na muda wa kushikana mashati na mpuuzi mmoja anayefanya upuuzi na mpuuzi mwinzie. Kwa kijana mwenye akili hapo ndio utakuwa mwisho wa hayo mahusiano yaliyokuwa yamejaa udanganyifu bila yeye kujua.

Vinginevyo labda mlikuwa wachumba huku mnaendelea kufanya uasherati, hapa haitakuwa ngumu kwa mmoja wenu kutembea na mwingine na mwingine. Usishangae, kama ameruhusu ulale naye atashindwaje kuruhusu alale na mwingine, kama ameshindwa kuvumilia mpaka mfunge ndoa atawezaje kuvumilia ukiwa naye mbali kidogo, kama ameshindwa kukuheshimu akafunilia uchi wake atashindwaje kumfunua/kufunulia na mwingine.

Mchezo wa mtu asiyejiheshimu huwezi kubadilishwa na kumpa ruhusa ya kulala naye, hata kama ukeshe naye usiku kucha mkifanya naye uashereti. Ukimpa mgongo tu kidogo atamwingiza mwingine ndani kwa tendo lile lile mlilofanya naye usiku kucha.

Nitakushangaa sana wewe upo siriaz kabisa na Mungu wako alafu unagombana na wadada/wakaka unaowafuma na huyo mchumba wako. Ndugu yangu unayoyaona leo kwa mchumba wako usifikiri utaweza kumbadilisha mkiwa naye ndani kama mke na mume, nakwambia unajidanganya.

Kama msomaji wa biblia mzuri utakuwa unaijua habari ya Yusuf na Mariam aliyemzaa Yesu, Yusuf baada ya kuona mpenzi wake ana mimba na wakati hawajafanya naye tendo la ndoa aliazimia kumwacha kwa siri.

Rejea;Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri. Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. MT. 1:18‭-‬20 SUV.

Leo hii wewe unamkuta mchumba wako yupo na mtu mwingine tena ukathibitisha kuwa wanafanya naye mapenzi, unaanza kupigana naye au unaanza kuleteana fujo kuonyesha wewe ni mmiliki wa huyo kaka/dada. Nakushauri hayo mambo waachie makahaba/malaya, wewe ni nafasi yako ya kuchukua kilicho chako na kutimua mbio.

Mwana wa Mungu hawezi kupigana kwa sababu amemkuta mchumba wake yupo na mwanaume/mwanamke mwingine, haipo kabisa. Labda uwe ulikuwa hutaki kupata mume/mke aliye wako peke yako. Kama una moyo huo wa mke wako kutembea na wanaume wengine nje na wewe itakuwa ni wewe. Na kama una moyo wa kumwona mume wako akiwa na wanawake wengine tena wakati mwingine wanalalia kitanda kile kile mnacholala naye, basi hiyo ni juu yako. Ila usije ukaanza kusumbua watu wakusaidie.

Usihangaike kabisa wala usirushe mkono wako kumpiga huyo anayetembea na huyo uliyekuwa unamwita mchumba wako, wala usirushe mkono kwa huyo mchumba wako kwa kumkuta akifanya vitendo viovu. Agana naye kwa wema kabisa na tangaza uamzi wako kwa familia yako na ya kwake kama mlishafika huko, alafu wewe endelea kumwomba Mungu akupe mwingine.

Mpaka hapo utakuwa umenielewa vizuri kaka/dada yangu, usijaribu kucheza na hili eneo litakupoteza na kuzima ndoto zako bila kuelewa ilikuwaje. Uwe makini sana unapokuwa kwenye uchumba, huo ndio wakati wako wa kumfahamu vizuri unayeenda kuishi naye. Na sio wakati wa kufanya naye mapenzi, ukianza kufanya naye mapenzi unamwondoa Mungu katika uchumba wenu.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, kwa ushauri na maombi wasiliana nasi kwa namba hizo hapo chini au unaweza kutushirikisha maoni yako kwa ku comment hapo chini au kutuandikia sms kwa namba hizo chini.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.