Fanya kazi kwa bidii sana, sio bidii tu, kwa moyo wako wote, kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.

Usifanye kazi kama unalazimishwa na mtu, fanya hiyo kazi vizuri uliyopata nafasi ya kuifanya, ifanye kwa uaminifu mkubwa.

Kama huwezi kuifanya kwa ubora ni vizuri ukatafuta kazi nyingine, kuliko kufanya kitu ambacho hukifurahii. Hata kama hukifurahii sana, kama umepata nafasi ya kukifanya, basi jilazimishe kukifanya kwa bidii ili kupata matokeo mazuri.

Pamoja na hayo yote, kufanya kazi kwa bidii, kupata pesa nyingi, kujenga nyumba nzuri, kusoma vizuri, na kuwa na mambo mengine mazuri ya kimwili. Usije ukajisahau hili la Mungu.

Usimsahau Mungu wako, hakikisha uhusiano wako na Mungu upo vizuri kabisa. Usihaingaike sana na mambo ya mwili ukamwondoa Mungu kwenye ratiba zako.

Hayo yote unayoyatafuta kwa bidii, Mungu akiamua usile matunda yake, hutokula, kwa hiyo huna haja kuwa jeuri. Huna haja ya kumwacha Mungu kwa sababu ya mafanikio yako.

Unaweza kujenga nyumba nzuri sana, lakini unaweza usikae au usiishi humo ndani. Kwanini usiishi? Baada ya kujenga tu unakufa.

Unaweza ukasoma vizuri kabisa, na usije ukavuna matunda ya kusoma kwako, Mungu akawa amekuita.

Muhimu sana kuzingatia haya, kama unafanya mambo makubwa sana, alafu eneo lako la kiroho lipo hovyo. Hakikisha unajiweka vizuri, uhusiano wako uwe vizuri.

Rejea: Na huko utajiri wao utakuwa mateka, na nyumba zao zitakuwa ukiwa; naam, watajenga nyumba, lakini hawatakaa ndani yake; nao watapanda mizabibu, lakini hawatakunywa divai yake. SEF. 1:13 SUV.

Ndugu yangu, angalia sana usije ukawa unapambana sana usiku na mchana, alafu wanaokuja kula jasho lako ni watu wengine kabisa. Wakati huo wewe upo kaburini, usiruhusu hilo litokee kwako.

Jenga uhusiano wako na Mungu, mafanikio yako yasikutenganishe na Mungu wako, kutafuta kwako maisha kusikutenge na Mungu wako. Hakikisha katika kutafuta kwako, Mungu anakuwa wa kwanza kwa kila hatua zako.

Mungu atusaidie sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.