Sijui unasumbuliwa na jambo gani katika maisha yako, unajua mwenyewe jinsi gani unapita kwenye tanuru hilo la moto. Watu wanaweza kukutazama kwa nje wakajua huna shida yeyote ila moyoni mwako unajua pito unalopitia.
Sijui umefika mahali gani ukasema basi nilipofikia nasubiria Mungu aje achukue roho yangu, unaweza ukawa umefikia hapo kutokana na hali uliyonayo sasa. Kuna wapo wanaweza kuonyesha wapo upande wako, na inawezekana pia wapo wanaotamani ufe kabisa.
Kuchoka kwako, na kufika kwako mahali ukasema wewe ni wa kufa tu, hakuwezi kubadilisha ukweli wa hichi ninachoenda kukueleza hapa, na wakati huu.
Haijalishi unaona nini kwako, haijalishi umeomba sana, haijalishi umeombewa sana, na haijalishi umeshauriwa sana. Hayo yote yameshindikana kukusaidia hali yako unayopitia, hayo yameshindwa kukuondoa kwenye tabu yako.
Leo unao uchanguzi mmoja tu, bila kutazama umejaribu mara ngapi, wala bila kuwaza unajionaje kwenye mwili wako, wala bila kujalisha unaionaje ndoa yako, wala bila kujalisha unaouonaje ugonjwa wako, wala bila kujalisha ugumba/utasa wako.
Haijalishi madaktari bingwa wametamka nini juu ya afya yako, haijalishi umekutana na wanasaikolojia wa viwango vya juu kiasi gani wameshindwa kukurejesha kwenye hali yako.
Jibu ni moja tu, nenda mbele za Mungu kwa kinywa chako mwenyewe, wala usitafute mtu akuombee. Nenda mbele za Mungu kwa imani, eleza kwa maelezo ya kawaida kabisa, usitafute maneno mazuri na bora sana ya kufikirika.
Vile unajisikia moyoni mwako, vile unaona shida inayokutesa kwenye mwili wako, vile unaona ndoa yako imekuwa mwiba kwako, vile unaona umehangaika sana kutafuta mtoto, vile unaona kila mwanaume aliyekuja kwako kutaka kukuoa. Badala ya kukuoa alikuachia jeraha la moyo wako, ukipiga hesabu ya majeraha yako uliyojeruhiwa na wachumba waliopita kwako, unajisikia kulia tu.
Mweleze Yesu Kristo hivyo hivyo unavyojisikia, ongea kama unaongea na rafiki yako unayemwamini sana Kumshirikisha mambo yako. Ongea kama unaongea na mzazi wako unayetegemea atakusaidia.
Usitafute maneno zaidi, hayo hayo maneno mweleze Mungu wako, najua utasema mtumishi nimeomba sana. Sio kuomba tu nimelia sana juu ya shida yangu, lakini sijapata suluhisho la mateso ninayopitia.
Sikia Neno la Mungu linasema nini juu ya maisha yako, usiamini sana maneno yangu, amini Neno linalotoka kwenye kinywa cha Mungu mwenyewe.
Rejea: Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua. YER. 33:3 SUV.
Huenda umeusoma sana huo mstari, huenda umeuimba sana huo mstari, leo Mungu anasema na wewe kwa namna isiyo ya mazoea, wala kawaida. Ukiweka imani yako sawa sawa, unaenda kubadilisha historia ya maisha yako siku ya leo, nakueleza kitu ambacho halisi kabisa.
Ufahamu wako ufunguliwe sasa uweze kuona siri kubwa iliyopo ndani ya mstari huu, ni mstari uliobeba muujiza wako. Huhitaji kuombewa na nabii, na mtume, wala na mchungaji wako, nenda mwenyewe mbele za Mungu.
Usiache kumshukuru Mungu kwa alichokutendea katika maisha yako, baada ya kusoma ujumbe huu.
Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu.
WhatsApp: +255759808081