Tabia ya kuchoka kusubiri kile Mungu alituahidia katika maisha yetu, huwa inakumbuka tulio wengi, na tabia ya kuchoka kumwomba Mungu kwa kile alituahidia atatupa. Ama kile tunajua tukienda kwake yeye anaweza kutusaidia, huwa tunaanza kukata tamaa pale tunapoona anachelewa kutujibu.

Bila kujua kuwa Mungu huwa hakawii kutimiza ahadi yake kwetu, kama tunavyodhania sisi Mungu anakawia.

Rejea: Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba. 2 Petro 3:9 SUV.

Mara nyingi tunafika mahali tunaona Mungu hawezi kutujibu tena lile hitaji letu tulilopeleka kwake, hii inatufanya tuanze kutoka nje ya njia yake.

Tunapotoka nje ya njia yake, badala yake tunakuwa tumepata hasara zaidi, laiti tungejua tunachopaswa kufanya, tusingeona Mungu kachelewa kutujibu maombi yetu.

Upo umhimu mkubwa sana kulijua Neno la Mungu, maana litakusaidia kufahamu mambo ya msingi, yatakayokusaidia kusimama katika zamu yako bila kuchoka.

Hatupaswi kuchoka kuendelea kumkumbusha Bwana, hadi pale utakapoona ametimiza ahadi yake kwako/kwetu. Kama aliahidi kukuponya, hakikisha unapokea uponyaji wako.

Kama aliahidi kukubariki, hakikisha unasimama kwenye ahadi hiyo, hadi uone anakubariki zile baraka alizokuahidia kukubariki.

Kama alisema mke/mume mwema anatoka kwake, hakikisha unakaa kwenye njia yake, hadi anakupa hicho kilicho chema. Bila kuchoka, wala bila kufikiri amechelewa sana kukupa.

Usifike mahali ukaanza kuona ahadi za Mungu ni za uongo, Mungu si mwanadamu hata aseme uongo. Akisema amesema, ni wewe kuendelea kumkumbusha bila kuchoka.

Rejea: Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza? Hesabu 23:19 SUV.

Ikiwa ulimwomba sana Mungu jambo fulani akutendee, ukafika mahali ukakata tamaa, kuanzia leo unapaswa kurudi tena kwenye mstari wa Mungu. Tena unapaswa kutubu kwa kosa la kukata tamaa, maana katika kukata tamaa upo uasi ndani yake ulifanyika kwako.

Usiache kumkumbusha Bwana mpaka pale utakapoona ametimiza ahadi zake kwako, usianze kufikiri Mungu huwa anawajibu watu fulani tu. Hata kwako anaweza kujibu hitaji lako.

Rejea: Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha BWANA, msiwe na kimya; wala msimwache akae kimya, mpaka atakapoufanya imara Yerusalemu, na kuufanya kuwa sifa duniani. ISA. 62:6‭-‬7 SUV.

Hapa Neno la Mungu linasema, msiwe na kimya, wala msimwache akae kimya, mpaka atakapoufanya imara Yerusalem. Hapa Mungu alikusudia kuubariki Yerusalem, walinzi wake wakaambiwa wasikae kimya, wala wasimwache Mungu akae kimya.

Hata kwako leo, Usiache kumbusha Bwana juu ya hitaji lako kwake, kama mwaka jana uliomba sana bila kuona matokeo. Na mwaka huu usiache kuomba, haijalishi miaka mingi imepita, endelea kumkumbusha Bwana.

Usiwe mtu wa kutangatanga bila sababu, kaa tulia usubiri ahadi za Mungu, na kweli Mungu atakujibu sawa sawa na mapenzi yake. Tena kwa wakati sahihi aliokusudia kwako kukujibu hitaji lako, cha msingi ni kutulia kwenye njia yake.

Mungu akubariki sana.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.