Matisho katika maisha yapo, yanaweza yakawa ni matisho ya kukufanya uwe na adabu kwa Mungu au mwanadamu.

Matisho haya yanaweza yakawa na nia njema ya kukuweka katika njia nzuri ya kumpendeza Bwana.

Maana wapo watu hawawezi kumheshimu Mungu hadi waone kuna tukio fulani la kuwaogopesha kwao, ndio waanze kumwona Mungu kwa viwango vya juu.

Matisho mengine yanaweza yakawa yana makusudi ya kumwona Mungu wako wa kweli hawezi kukusaidia katika maisha yako ya wokovu.

Sijui kama unanielewa ninaposema matisho, hizi ni kauli za kukufanya ujione si kitu. Ama ni kauli za kukudharau kwa kukuonyesha huwezi kufanya chochote katika jambo fulani.

Sasa wapo watu kupitia miungu yao, huwa wanawatishia watu amani na kuwaonyesha kuwa watawafanya kitu kibaya cha kuwadhuru.

Wanasahau kuwa watumishi wa Mungu wa kweli, ama wana wa Mungu wa kweli. Nikiwa na maana wanaoishi maisha matakatifu ya kumpendeza Mungu, hao hawezi kupata shida na matisho hayo.

Kama nilivyotangulia kusema hapo awali kuwa matisho yapo kabisa, unaweza kukutana nayo katika huduma yako. Lakini ukijua uliyenaye ni nani ndani yako, na ukijua uliitwa na nani, hakuna jambo litakuyubisha.

Hili tunajifunza kwa mtumishi wa Mungu Hezekia, aliletewa ujumbe wa matisho mabaya na Senakeribu.

Rejea: Mwambieni Hezekia, mfalme wa Yuda, maneno haya, mkisema, Asikudanganye Mungu wako unayemtumaini, akisema, Yerusalemu hautatiwa katika mikono ya mfalme wa Ashuru. Tazama, umesikia ni mambo gani wafalme wa Ashuru waliyozitenda nchi zote, kwa kuziangamiza kabisa; je! Utaokoka wewe? 2 FAL. 19:10‭-‬11 SUV.

Huu ujumbe ukikujia ukiwa kwenye wakati fulani, unaweza ukakupa shida kubwa sana katika moyo wako.

Pamoja na kukupa shida, unapaswa kuelewa ni mahali gani pa kukimbilia wewe ili uwe na salama.

Usifikiri kila kitisho huwa wanaongea kwa kubahatisha, mtu anakuwa ana uhakika na anachokiongea. Usipokuwa vizuri kiroho anakudhuru kweli.

Tunamwona mtumishi wa Mungu Hezekia, baada ya kuletewa ujumbe wa maneno makali ya kutishia uhai.

Tunamwona alichukua hatua ambayo sio kila mtu anaweza kukumbuka haraka kujua ndio njia yake ya pekee kumponya.

Rejea: Naye Hezekia akaomba mbele za BWANA, akasema, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, ukaaye juu ya makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia; wewe ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi. Tega sikio lako, Ee BWANA, usikie; fumbua macho yako, Ee BWANA, uone; uyasikie maneno ya Senakeribu, ambayo amemtuma mtu aje nayo ili kumtukana Mungu aliye hai. 2 FAL. 19:15‭-‬16 SUV.

Unaona kile ambacho anapaswa kufanya mtumishi wa Mungu, Hezekia baada ya kupokea waraka wa Senakeribu, alichukua hatua ya kumwendea Mungu.

Tunaona maombi yake yakiwa kipaumbele chake, hakubaki kulalamika, hakubaki na hofu. Alichukua hatua ya kumweleza Baba yake wa mbinguni.

Nasi tunapaswa kuiga mfano huu bora kabisa wa Hezekia tukiwa kama wa Mungu aliye hai, yapo matisho ya watu wasio na Mungu wa kweli tunakutana nayo katika kazi zetu, biashara zetu, huduma zetu, shule zetu, na vyuo vyetu.

Ukikutana nayo yasiwe shida kwako kiasi kwamba unaanza kufikiri kufanya jambo lisilofaa katika maisha yako ya wokovu.

Haya ndio majibu ya Mungu kwa mtu ambaye anamwomba amsaidie katika shida yake aliyonayo wakati huo.

Rejea: Basi BWANA asema hivi katika habari za mfalme wa Ashuru, Yeye hatauingia mji huu, wala hatapiga mshale hapa, wala hatakuja mbele yake kwa ngao, wala hatajenga boma juu yake. Njia ile ile aliyojia, kwa njia iyo hiyo atarudi zake, wala hataingia ndani ya mji huu, asema BWANA. Maana nitaulinda mji huu, niuokoe, kwa ajili yangu mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi wangu. 2 FAL. 19:32‭-‬34 SUV.

Haya ni majibu ya Mungu kwa mtoto wake aliyetishiwa uhai wake na mtu asiyemjua Mungu wa kweli.

Hata kwako inawezekana kabisa, usiogope vitisho, nenda mbele za Mungu atakusaidia na mambo yote yakuwa sawa.

Mungu atusaidie sana.
Samson Ernest
+255759808081