Katika vitu ambavyo huwa tunakosea na tunatumia nguvu nyingi ni kupambana kwa nguvu kuitaka nafasi fulani au eneo fulani kuwa miliki yako.

Bila kujua hiyo nafasi au hilo eneo Mungu amekupa liwe lako au Mungu amekuhakikishia ni halali yako?

Inawezekana kabisa ni wakati wako umefika, lakini hilo unaloliona linapaswa liwe la kwako. Inawezekana kabisa si la kwako.

Nafasi unaiona ipo wazi kabisa na wewe ni muhitaji wa nafasi hiyo, pamoja na muhitaji inawezekana kabisa mwenye nafasi hiyo sio wewe ni mwingine kabisa.

Ni muhimu sana kulijua hili, neno la Mungu linapaswa kuwa kwa wingi ndani yako. Ili Roho Mtakatifu anavyokusemesha uwe unamwelewa kirahisi.

Hili tunaliona kupitia maandiko matakatifu, Bwana anavyokuwa wazi kwa watu wake.

Rejea: BWANA akaniambia, usiwasumbue Wamoabi, wala usishindane nao katika mapigano; kwa kuwa sitakupa katika nchi yake kuimiliki; kwa sababu Ari nimewapa wana wa Lutu kuimiliki. KUM. 2:9 SUV.

Ushindane na mtu, sikiliza kwanza Mungu anasema nini. Unaweza kushindana naye ukawa unapoteza nguvu zako bure kwa kitu ambacho sio cha kwako.

Usihangaikie nafasi unayoitaka wewe bila kumsikiliza Mungu anasemaje kuhusu hiyo nafasi.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.