Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, habari za muda huu ndugu yangu, ni wasaa mwingine tena wa kwenda kushirikishana yale tuliyojifunza katika sura ya leo.

Hebu tujifunze kuhusu kufuata maagizo, ili tuweze kufanikiwa katika eneo fulani tunapaswa kufuata kanuni zilizowekwa. Na ili tuweze kukosea njia inayotufikisha kwenye lengo, tusifuate yale tuliyoelekezwa.

Unapoenda kinyume na taratibu zilizowekwa mahali, unataka kugombana na eneo husika. Na unapoenda sawasawa na taratibu zilizowekwa utaendana vizuri, na watu bila tatizo lolote, na mtu.

Sawa na mtu aliyepangiwa majukum yake ya kazi, anapoyatekeleza kwa uaminifu, kiongozi wake hana haja ya kugombana naye. Shida inakuja pale mtu anapopangiwa la kufanya alafu asifanye vizuri.

Hata sisi tulioajiri watu wa kutusaidia majukum yetu, pale wanaposhindwa kuyatimiza majukum yao. Wakati mwingine huwa wakali sana kwao, maana hawajatimiza wajibu wao.

Tujifunze kusimama katika nafasi zetu, tunaposimama katika nafasi zetu tutafanya vizuri bila kusukumwa na mtu yeyote. Tunavyoendelea kutekeleza wajibu wetu inatuweka nafasi nzuri, na inasababisha wanaotuzunguka waone mchango wetu kwao.

Kutekeleza majukum sio jambo la ajabu sana, ni vile unavyosimama kwenye zamu yako, ndivyo unavyozidi kuwavuta wengi sana kukupenda. Sio wanakupenda kwa sababu una sura nzuri, wanakupenda kwa sababu unawajibika katika nafasi yako uliyowekwa.

Najua hata nyumbani kwako kama una watoto, unamfurahia sana yule mtoto anayefanya vizuri na kuzingatia yale unayomwagiza. Na unakuwa mtoa adhabu kwa yule mtoto mtukutu asiyependa kutekeleza yale unayomwagiza.

Vilevile kwenye ndoa, mwanaume asiyetekeleza wajibu wake ni mzigo kwa mke wake na watoto wake. Na mwanamke asiyesimama kwenye nafasi yake anasababisha kuanzisha vitu visivyo na maana kwa mume wake.

Lakini tunaposimama kwenye nafasi zetu, tunakuwa sehemu ya kutoa mchango mkubwa kwa wahitaji wa huduma tunazotoa kwao. Tunapofanya tunazidi kujiweka katika nafasi nzuri ya kuaminika kwa familia zetu na jamii inayotuzunguka.

Inafika mahali watu wanahitaji mtu wa kusimamia jambo, wanaangalia mtu makini na mwenye kujituma wanamkosa. Ila wanapokuja kwako wanaona unafaa kwa sababu ya vile unavyojituma.

Kujituma kwetu kunatuweka kwenye nafasi nzuri sana, nje na kuwa tunalipwa kwa kile tunachotoa au tunachofanya. Hebu ujiuliza una mchango gani kwa kile ulichokabidhiwa ukifanye, je watu wanafurahia huduma yako? Je wapo tayari kusimama kifua mbele kukutetea hata kama ulikosea kidogo?

Ikiwa upo kazini ukiondoka kwenda likizo wala watu hawajui kama umeondoka, ujue una mchango mdogo sana ambao haugusi maisha ya wengine. Ikiwa utaondoka sehemu watu wanasema bora ameondoka, ujue ulikuwa huna mchango wowote juu ya maisha yao.

Umewahi kuona mwalimu anahama shule moja kwenda nyingine, wanafunzi wanalia machozi mpaka wengine wanaenda kulala barabarani ili gari lisiweze kuondoka!
Kama hujawahi kuona basi ujue imewahi tokea shule zingine, si kwa sababu ya kitu kingine bali ni ule mchango wake kwao.

Kuna mtu hajanipata vizuri ninachosema hapa, najua unamkumbuka Doricas baada ya kufa, kile alichokifanya kwa wamama wenzake akiwa hai, ndicho kilichomsababisha arudishiwe tena uhai wake.

Nazungumzia kuhusu kuwajibika kwenye nafasi yako ili kuepuka kugombana na watu, na kujisababishia baraka kwa wengine, kwa sababu ya kusimama katika nafasi yako, si kwa hila bali ni kwa Upendo.

Tunajifunza kwa watu hawa waliopewa kazi na mfalme Suleiman, walisimama vyema na kutekeleza wajibu wao.

Rejea: Wala hawakuyaacha maagizo ya mfalme aliyowaamuru makuhani na Walawi kwa neno lo lote, wala kwa habari ya hazina. 2 NYA. 8:15 SUV.

Unasimamia vipi rasilimali ulizokabidhiwa uzisimamie, unapaswa kujiuliza hili na kulifanyia kazi, ili uone mafanikio ya kazi uliyopewa au unayofanya wewe binafsi.

Tengeneza sifa njema kwa kila nafasi unayopewa na uliyopo, hata ikitokea unaondolewa mahali watu waseme hakika huyu hasitahili kuondoka/kuondolewa. Kelele zao zinaweza kukuokoa kwenye hatari iliyosimama mbele yako, ni hatari sana kila mtu kutoona mchango wako katika nafasi uliyopo sasa na uliyopita.

Tunajua hatuwezi kumpendeza kila mtu ila tufahamu kwamba, michango yetu tunayotoa kwa wengine inaonekana sana katika familia na jamii inayotuzunguka.

Ili tusaidike na hili, tuwe watu wa kuzingatia wajibu wetu tuliopewa, kutimiza kwako majukum uliyopewa, inakufanya uwe katika nafasi nzuri.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu
+255759808081.
www.chapeotz.com