“Esau akawatwaa wakeze, na wanawe, na binti zake, na watu wote wa nyumbani mwake, na ng’ombe zake, na wanyama wake wote, na mali yake yote, aliyoyapata katika nchi ya Kanaani; akaenda mpaka nchi iliyo mbali na Yakobo nduguye. Maana mali yao yalikuwa mengi wasiweze kukaa pamoja, wala haikuweza nchi ya kusafiri kwao kuwachukua, kwa sababu ya wanyama wao”, Mwa 36:6‭-‬7 SUV.

Esau alifanikiwa sana kwenye Mali, alifanikiwa kumiliki Mali nyingi kiasi kwamba alikosa nafasi ya kuendelea kuishi eneo moja na ndugu yake Yakobo.

Jambo linalosikitisha kwa Esau ni hili, alifanikiwa sana kuwa na Mali nyingi ila eneo la kiroho alikuwa chini, hakuwa na mafanikio yeyote ya kiroho.

Alijali sana Mali zake, lakini hakujali mambo ya kiroho, akawa mtu aliyefanikiwa kimwili ila kiroho akawa sifuri kabisa.

Tunaona hili alilianza zamani kipindi tumeona anauza uzaliwa wake wa kwanza kwa njaa iliyompata wakati huo. Huku ni kutokujali mambo ya muhimu.

“Yakobo akampa Esau mkate na chakula cha dengu, naye akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza”, Mwa 25:34 SUV

Matokeo ya kudharau kwake mambo ya msingi, tunaona taifa alilolianzisha, taifa la Edomu, halikumcha Mungu kabisa.

Kutomcha Mungu kwa Edomu kulisababisha ghadhabu ya Mungu kwa taifa hilo.

“Nao watashuka, watalirukia bega la Wafilisti upande wa magharibi; nao pamoja watawateka wana wa mashariki; watanyosha mkono juu ya Edomu na Moabu; na wana wa Amoni watawatii”, Isa 11:14 SUV.

Unaweza kuona ni jinsi gani mtu anaweza akawa na Mali nyingi ila akawa hana habari na Mungu, kitendo ambacho kinaweza kusababisha madhara kwa mtu huyo.

Mtu asiyejali mambo ya Mungu, anaweza kufanya mambo yasiyofaa mbele za Mungu, kwa sababu hofu ya Mungu haimo ndani yake.

Mafanikio yetu ya kimwili yasitufanye tukamwacha Yesu, tukaendelea na mambo yetu mengine. Tunaweza kusababisha shida kubwa kwenye familia zetu.

Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia yako
Mungu akubariki sana
Samson Ernest