Sijui unakumbuka nini kibaya ulichowahi kufanya huko nyuma, ambacho kinakufanya ukose amani ya moyo wako.

Huenda unakumbuka dhambi zako ulizowahi kufanya kipindi cha nyuma kabla ya kuokoka. Ambazo zinakufanya ukose ujasiri wa kumshuhudia Yesu Kristo, alivyokuokoa.

Huenda unakumbuka ulivyokuwa malaya, ukikumbuka hayo unakosa kabisa ujasiri wa kumshuhudia Yesu Kristo, kwa yule ambaye bado hajamjua Kristo.

Huenda bado unakumbuka ulivyozaa mtoto nje ya ndoa yako, umeokoka lakini bado unateswa na hiyo kumbukumbu mbaya, na tena umeolewa ila bado unajiona u mkosaji.

Sikiliza Neno la Mungu siku ya leo, linasema usiyakumbuke hayo yote;

Rejea: Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani. ISA. 43:18 SUV.

Kuendelea kukumbuka mambo ya nyuma, ni kuendelea kuutesa moyo wako, amini Mungu ameshakusemehe kabisa makosa yako.

Mungu akishasema amekusamehe, amini amekusamehe kweli, hakuna kufikiri kitu kingine zaidi ya msamaha wa Mungu kwako.

Tena anasema mwenyewe, hebu ona kupitia andiko hili;

Rejea: Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako. ISA. 43:25 SUV.

Mungu anasema hatazikumbuka dhambi zako, tena anaongeza zaidi kwa kusema, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe.

Mungu anayafuta makosa yako kwa ajili yake mwenyewe, wewe kuendelea kuteswa na mambo ya zamani, ni kwa sababu hukufahamu hili andiko lake takatifu.

Hupaswi kuendelea kuteswa na kumbukumbu mbaya kwenye ufahamu wako, kazi yako ni kumtumikia Mungu wako katika roho na kweli.

Usiteswe na mambo mabaya ya zamani, kama hukuenenda vizuri siku za nyuma katika ujana wako. Na sasa umeamua kuenenda pamoja na Yesu Kristo, huna haja ya kuruhusu fikra potofu zikutese.

Zamani uliteswa sana na mahusiano mabovu, na sasa upo kwenye mahusiano mazuri, acha kuteswa na kumbukumbu za zamani.

Ulikutana na mwanaume akuumiza moyo wako, usiweke akilini mwako wanaume wote ndivyo walivyo. Ukashindwa kumpenda uliyenaye sasa, kwa sababu ya kumbukumbu mbaya za nyuma.

Ulikutana na mwanamke akakutenda vibaya kabla hajawa mke wako wa ndoa, usijenge fikira potofu kwa uliyenaye sasa. Kwa kukumbuka mambo mabaya ya zamani.

Kukumbuka mambo ya zamani ukiwa umeokoka, huo ni uchanga wa kiroho, mtu anayelijua Neno la Mungu. Hawezi kuteswa na mambo ya zamani, kwanza atateswaje na wakati Mungu ameshamwambia kupitia Neno lake kuwa amemsamehe!

Ukishakuwa ndani ya Yesu Kristo, umefanyika kiumbe kipya, acha kuwa mnyonge kwa sababu ya mambo ya zamani uliyowahi kuyafanya.

Je, unapenda kukua kiroho kwa kusoma Neno la Mungu kila siku? Karibu sana group la WhatsApp, tuwasiliane kwa namba hizo chini.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Website: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081