Zipo taarifa nyeti zinazokuhusu wewe zinaweza kukufikia kwa siri, na wanaokufikishia hizo taarifa wakawa ni watu wako wa karibu sana.

Kwa namna yeyote ile, ukazichukulia kawaida, ama ukazipuuza kutokana na jinsi unavyojiamini wewe kama wewe.

Kuzipuuza kwako hizo taarifa mbaya, baadaye zikaja kukuletea madhara makubwa wakati ulikuwa na nafasi kubwa ya kuweza kuepukana na hayo yaliyokukuta.

Mfano mzuri ni humu(group la WhatsApp), huwa kuna taarifa nyeti huwa nazipata, kisha nazifanyia kazi, na kweli baadaye matokeo ya taarifa zile yanakuja kuonekana wazi.

Ningekuwa nazipuuza, ningevuruga group hili kwa kutotilia maanani taarifa muhimu ninazozipata kwa watu waaminifu.

Hili la kupuuza taarifa mbaya, lilimkuta Gedalia, Gedalia alipewa taarifa mapema na watu wake wa karibu kuwa anatafutwa auawe. Yeye akaona aliyeleta taarifa anamsigizia Ishmael. Ambaye Ishmael ndiye aliyekuwa muuaji.

Rejea: Wakamwambia, Je! Una habari wewe ya kuwa Baalisi, mfalme wa wana wa Amoni, amemtuma Ishmaeli mwana wa Nethania, akuue? Lakini Gedalia, mwana wa Ahikamu, hakusadiki neno hili. YER. 40:14 SUV.

Sikufundishi uwe unahangaika kutafuta taarifa mbaya juu yako, ninachosema hapa ni pale unaletewa taarifa mbaya zinazohatarisha uhai wako. Alafu hizo taarifa ukazipuuza kwa namna yeyote ile, yanaweza kutokea madhara mabaya kwako.

Ukifuatilia hii habari katika sura ya 41, utaona Gedalia akiuawa na Ishmael, yule aliyempuuza na kumwona anasingiziwa mabaya. Ndiye aliyemtoa uhai wake, angesikiliza ushauri wa mwanzo huenda angeweza kuepuka hicho kifo.

Rejea: Akaondoka huyo Ishmaeli, mwana wa Nethania, na watu wale kumi waliokuwa pamoja naye, wakampiga Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, kwa upanga, wakamwua; yeye ambaye mfalme wa Babeli amemweka kuwa liwali wa nchi. Tena Ishmaeli akawaua Wayahudi wote waliokuwa pamoja naye, yaani, pamoja na Gedalia, huko Mizpa, na hao Wakaldayo walioonekana huko, yaani, watu wa vita. YER. 41:2‭-‬3 SUV.

Sijui umewahi kupuuza taarifa mbaya ngapi kwako, ila fahamu siku zote, hupaswi kupuuza taarifa zozote mbaya bila kuzifanyia uchunguzi. Vizuri kusikiliza na kuzifanyia kazi, ikiwezekana ingia kwenye kumwomba Mungu akuepushe na baya hilo.

Ester angepuuza taarifa za kuuawa kwa taifa lake, wangeuawa kweli ila alichukua hatua na kuingia kwenye maombi ya kufunga siku tatu.

Leo unaweza kuletewa taarifa mbaya ukaona ni za kukuchonganisha na mume/mke wako. Kabla hujazipuuza zifanyie kazi taratibu kujua ukweli wake, ukishaona hazina ukweli achana nazo.

Unaweza ukazipuuzia kumbe zikawa zina ukweli ndani yake, ungezichukulia hatua mapema ungeweza kuepusha mengi kwenye ndoa yako.

Unaweza kupata taarifa mbaya kuhusu mchumba wako, ukaona watu wana wivu juu ya uhusiano wako. Ukaacha kuzifanyia kazi zile taarifa ulizopewa, kumbe zilikuwa na ukweli. Ukawa umejiingiza kwenye madhara ambayo ungeweza kuyaepuka mapema kabla ya kuingia kwenye ndoa.

Vizuri kusikiliza na kuwa na chujio lenye uwezo wa kuchuja taarifa feki na halisi, vinginevyo unaweza ukajiingiza kwenye jambo baya kwa ukaidi wako wa moyo.

Gedalia alimwona Ishmael anasigiziwa mabaya wakati yeye hana tabia hiyo mbaya. Ila mwisho wa siku yakamtokea mabaya, ambayo yaliondoa uhai wake.

Mungu atusaidie tuwe na sikio la kusikia taarifa zenye kusudio njema la kuokoa maisha yetu.

Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081