Utumishi wa Mungu ni kazi moja ngumu kwa upande mwingine, usipokuwa mwangalifu unaweza kusema utumishi basi.

Unaweza kuhubiri Neno la Mungu likawachukiza wakuu wasiomjua Mungu wa kweli, mahubiri yale yakakuletea shida kubwa kwenye utumishi wako.

Unaweza kujiingiza kwenye utumwa/ukimbizi wa nchi yako, kwa sababu ya kuisema kweli ya Mungu.

Unaweza ukawa mtu wa kujificha kwenye nchi yako, kwa sababu Mungu alikutuma ukaiseme kweli yake. Ili wale watakaosikia wapate kumrudia yeye.

Rejea: Ndipo hao wakuu wakamwambia Baruku, Enenda ukajifiche, wewe na Yeremia, wala mtu asipajue mlipo. YER. 36:19 SUV.

Baruku mwandishi aliyeandika unabii wa Yeremia kutoka kwa Mungu, na kuusoma unabii ule kwa watu wa Yuda. Wakuu waliona ni ujumbe ambao utawaletea shida, wakamwambia Baruku akajifiche na nabii Yeremia, mtu yeyote asijue walipojificha.

Kweli baada ya mfalme wa Yuda ambaye alikuwa Yehoyakimu, kusikia maneno yale, kwanza alichoma Gombo la Chuo. Baada ya kuchoma alianza kumtafuta mwandishi Baruku na nabii Yeremia, lakini hakuweza kuwapata.

Pamoja na mfalme Yehoyakimu kuchoma Gombo la Chuo, Mungu alisema tena na nabii Yeremia, aandike Gombo la chuo lingine maneno yale yale yaliyochomwa moto.

Rejea: Haya! Twaa wewe gombo lingine, ukaandike ndani yake maneno yote ya kwanza, yaliyokuwa katika gombo la kwanza, ambalo Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, ameliteketeza. YER. 36:28 SUV.

Hapa inatupa kuona kwamba, huwezi kuzimisha ukweli wa Mungu, huwezi kufuta agizo la Mungu aliloliagiza. Utajitahidi kupoteza ushahidi wa Neno la Mungu(unabii wake) lakini Mungu ataufufua tena.

Utajaribu kumuua mtumishi wa Mungu kwa kuusema ukweli wake, fahamu utakuwa umejiingiza kwenye hatia kubwa mbele za Mungu. Ila uwe na uhakika kwamba, Mungu atainua mtumishi mwingine wa kuisema kweli yake.

Tena tunajifunza kwamba, watumishi wa Mungu wanalindwa na Mungu mwenyewe. Watu kama mfalme Yehoyakimu wakijaribu kuuzimisha ukweli wa Mungu, hawataweza.

Rejea: Mfalme akamwamuru Yerameeli, mwana wa mfalme, na Seraya, mwana wa Azrieli, na Shelemia, mwana wa Abdeeli, wamkamate Baruku, mwandishi, na Yeremia, nabii; lakini BWANA aliwaficha. YER. 36:26 SUV.

Bwana atakuficha mtumishi wa Mungu, hubiri injili, sema kweli ya Mungu, haijalishi Mazingira, kama MUNGU amekutuma, hakikisha utekeleza agizo lake.

Tunajifunza kwa mwandishi huyu Baruku, na nabii Yeremia, waliusema ukweli wa Mungu, bila kujalisha mfalme atawaua.

Mungu akupe ujasiri.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com