“Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena”, Yn 6:66 SUV.
Yesu akiwa anajifafanua yeye ni nani, miongoni mwa watu waliomkimbia au kujiweka pembeni ni wanafunzi wake aliokuwa nao.
Ukaribu wa wanafunzi wake inaonyesha wazi bado walikuwa na maswali au mashaka yaliyokuwa yanawakabili.
Yesu alipojiweka wazi baadhi yao walirudi nyuma, kitendo ambacho kilimfanya Yesu awaulize hata ninyi mnanikimbia?
“Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! Ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu”, Yn 6:67-69 SUV.
Petro alikuwa mwepesi kujibu, na kusema kweli juu ya Yesu Kristo, lakini kabla ya hapo kulishatokea utengano kwa baadhi yao.
Nataka uone nini hapa, ukiwa kiongozi kuna wakati watu wako wa karibu wanaweza kujitenga nawe, sababu haswa inaweza ikawa kutokukuelewa.
Wakati mwingine hata familia yako, unaweza kutengwa nayo kutokana na maamuzi uliyochukua, wakija kukuelewa ndio wanakurudia na kuwa pamoja nao.
Tunahitaji kuelewa katika maisha haya upo wakati tunaweza kukimbiwa hata na wale tuliokuwa nao karibu. Kinachowakimbiza ni kutofautiana mtazamo au maono.
Kurudi nyuma kwa watu wako wa karibu kusikufanye uache kusudi la Mungu aliloweka ndani yako, songa mbele.
Ukifanya hayo utakuwa mtu bora katika utumishi wako, maana hutoyumba kwa sababu uliowaamini wamekukimbia au wameacha kushirikiana na wewe.
Soma neno ukue kiroho
Kwetu kusoma biblia ni maisha
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081