
Hakuna kisingizio chochote kwa mtu kusema Mungu hayupo, kama ni matendo makuu ya Mungu tunayaona kwa uwazi kabisa kupitia matendo yake makuu.
Tunaona miujiza mikubwa ya Mungu ikitendeka kwa uwazi kabisa, wapo walikuwa wagonjwa wa miaka mingi sana ila kupitia jina la Yesu Kristo walipokea uponyaji wao.
Tunaona wapo walikuwa wamefungwa matumbo yao ya uzazi, kupitia jina la Yesu Kristo matumbo yao ya utasa yalifunguliwa na kubeba ujazito, na watoto wakazaliwa wazuri.
Tunaona wapo watu walioshindikana kutokana na tabia zao mbaya, lakini Yesu Kristo alipoingia moyoni mwao, tabia zao zilibadilika na kuwa watu wazuri.
Tunaona watu walikuwa majambazi sugu ila walipompokea Yesu Kristo, waliachana na tabia hiyo mbaya.
Pamoja na hayo yote bado unaweza kutoa udhuru kuwa Mungu wa kweli hayupo, kupitia matendo hayo yote makuu bado unaona kuabudu sanamu au miungu mingine kunafaa sana?
Rejea: Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake; hata wasiwe na udhuru. RUM. 1:20 SUV.
Usiwe na udhuru wa aina yeyote, Mungu yupo, tunaona kazi zake, tunaona matendo yake, uhai tulionao ni yeye ametupa.
Huna udhuru kwamba hukusikia habari za Yesu Kristo, watumishi wa Mungu wamekuambia sana kuabudu sanamu ni dhambi, kuabudu miungu ya mababu zako ni dhambi. Utakuwa na udhuru tena wa kusema hukusikia habari kama hizo?
Hakuna udhuru, unajua ulevi ni mbaya, unajua ushoga ni mbaya, unajua uzinzi/uasherati ni mbaya, unajua mengi mengi sana. Watumishi wa Mungu wamehubiri na kufundisha sana, lakini umewapuuza.
Kuwa na udhuru sasa, ila siku ya mwisho huna utakalojitetea mbele za Mungu, kwa kifupi huna udhuru wowote wa kukufanya usiokoke au usiache hayo mabaya.
Kama bado hujajiunga na kundi la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, unakaribishwa sana ujiunge. Tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081 utaunganishwa.
Mungu akusaidie usiwe na udhuru.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com