“Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri?” Rum 10:14 SUV.

Imani yeyote unayoiona iwe nzuri au mbaya, ujue mtu aliibeba kwa kusikia mafundisho au mahubiri.

Mafundisho sahihi yanazalisha Imani sahihi, na mafundisho potofu yanazalisha Imani potofu.

Mtu anayesikiliza mafundisho sahihi mara kwa mara uwe na uhakika yatajenga Imani kwake.

Mtu anasikiliza sana mafundisho potofu kwa muda mrefu na akawa hana msingi mzuri wa neno la Mungu, uwe na uhakika mtu huyo atageuzwa moyo wake.

“Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo”, Rum 10:17 SUV.

Ukihitaji mtu awe na imani unayoona wewe ni sahihi, mpe mafundisho sahihi, mtu huyo ataishika imani yako.

Njia hii inatumika vibaya kwa watu wenye mafundisho potofu na Imani isiyo sahihi, wanapofundisha watu huishika Imani hiyo na kuanza kuiishi.

Tunapaswa kuwa makini na mafundisho mbalimbali kwa sababu kila fundisho hujenga au hubomoa msingi fulani wa Imani na kujenga mwingine.

Ukiwa unapata mafundisho sahihi itakuwa ni heri kwako, hata kama umeondolewa kwenye dini yako.

Hatari ni kuondolewa kwenye sehemu sahihi, na kwenda sehemu wanayoamini yasiyo sahihi.

Neno la Mungu ndio msingi wako mkuu wa mafundisho yeyote yale, fundisho lililo nje na neno la Mungu hilo ni sumu kwako.

Sio neno tu unahitaji kuwa na uelewa sahihi juu ya neno, ukiwa na mtazamo tofauti juu ya neno utalisoma na utalielekeza kwenye mtazamo wako potofu.

Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia
Mungu akubariki sana
Samson Ernest