Tupo duniani, tutaendelea kuona mengi, tutaendelea kusikia mengi, na tutaendelea kukutana na mengi. Hakuna kupumzika, leo utaona hili, kesho utasikia lile, kesho kutwa utakutana na lingine tofauti kabisa na la jana.

Usifikiri kwamba haya yataisha, kama unafikiri au unawaza changamoto zinazokubali leo zitaisha lini. Unapaswa kufahamu hili, mwisho wa changamoto moja, ni maandilizi ya changamoto nyingine mpya kabisa tofauti na siku nyingine.

Utachopaswa kufahamu, ni kuwa na moyo imara wa kuweza kukabiliana na kila changamoto inayokuja mbele yako. Na ili uweze kuwa na moyo imara, unapaswa kuwa na mahusiano imara na Mungu wako, maarifa kwako hayapaswi kukauka.

Leo utakuwa na nafasi nzuri kazini kwako, usifikiri umemaliza kila kitu, utakutana na changamoto ambazo hujawahi kuzifikiri kabisa zingekuja kwako. Wale unaowaogoza, itafika mahali watapanga mabaya juu yako, sio kwa sababu umeshindwa kuwaongoza, wataingiwa tu na roho mbaya.

Usishangae pamoja na kuwa mchungaji, mtume, nabii, mwinjilisti, na mwalimu, washirika wako au viongozi wenzako. Wakafika mahali wakapanga kukuondoa katika nafasi yako, wakapanga kukushambulia kwa maneno mabaya ya kukuumiza moyo wako.

Usipoyajua haya mapema, siku yakikupata unaweza kupata shida sana moyoni mwako. Utaanza kufikiri labda kuna mahali umemkosea Mungu wako, kumbe sio kweli umekosea Mungu wako, ni vile tu hawataki kuelezwa ukweli.

Ukiwa na msimamo mkali, na mtu mwenye kusimamia haki, mtu usiyependa kona kona zisizofaa, alafu ukikutana na watu wanaopenda kona kona mbaya. Lazima upishane nao, maana watataka kupitisha mambo yao mabaya na wewe utaweka kizuizi. Na hawataweza kufanya chochote maana wewe ndiye mtoa maamzi wa mwisho.

Wakishakuona umesimama imara, uwe na uhakika wote wasiopenda msimamo wako, wataanza kutafuta njia ya kukushusha kwenye kiti chako au nafasi yako.

Haya mambo hayajaanza leo, yalishatokea kwa nabii Yeremia, pamoja na kuwa nabii aliyetumiwa sana Mungu. Bado kuna watu walikaa vikao vya kupanga namna ya kumwangamiza kwa maneno yao.

Rejea: Hapo ndipo waliposema, Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yo yote. YER. 18:18 SUV.

Haijalishi watu wanaonyesha kukupenda sana, hilo lisikupe kiburi ukaacha kuweka nguvu zako kwa Mungu wako. Wakati wowote hao hao walionyesha kukupenda na kuwa upande wako, ipo siku watakugeuka mchana kweupe.

Tegemeo lako kuu liwe kwa Mungu wako, usije ukalewa sifa ukajaa kiburi kwa kufikiri unapendwa sana, hakuna wa kukupinga/kukuondoa. Hakuna kitu kama hicho, hata kama unamhubiri Mungu wa kweli, watafika mahali watasema unahubiri uongo.

Haijalishi umekuwa mwaminifu kwa muda mrefu sana mbele za Mungu, na umejaribu kuwapendeza wanadamu wenzako. Itafika mahali watapanga mabaya kwako, hili halitaaza kwako, yalishaanza kwa nabii Yeremia.

Mungu akubariki sana.
Soma Neno Ukue Kiroho.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.