Wapo wataalam wa kufunika mambo ili ionekane hakuna tatizo lolote, bali ionekane ipo amani ya kutosha. Hata kama kuna matatizo makubwa yanawakabili, hutakaa umwone akionyesha kwa wazi hana amani.
Kwa upande mwingine inaweza ikawa nzuri, hasa kwa adui yako ila sio mbele za Mungu. Adui yako unaweza kumnyima nafasi asione jinsi gani anayokutendea mabaya yanakuumiza moyo wako.
Utadanganya watu kwa nje, ndoa yako ina amani ya kutosha, kama ni kwenye mitandao ya kijamii utaweka picha za kila namna kuonyesha mna amani ya kutosha na mke/mume wako. Ila ukifika ndani kwako unatamani usilale humo, maana hapakaliki kabisa kila mtu na chumba chake, amani haipo.
Unaweza kuzuga mna mahusiano mazuri na mchumba wako, ili tu kuwaonyesha marafiki na ndugu zako. Ila huwezi kuondoa uhalisia uliopo kati yenu, kama amani haipo, itabaki haipo tu.
Unaweza kuwaonyesha ndugu zako, hamna tatizo na mume/mke wako, ukawajibu kwa namna ya kuwaonyesha mna amani na furaha kwenye ndoa yenu. Ila ukirudi kwenye uhalisia, kuna mahali unapitia pagumu sana kwenye mahusiano yako ya ndoa.
Unaweza kuonyesha watu kwa nje, biashara zako zinaenda vizuri sana, na zinakua zaidi. Kumbe ni uongo, wanachoona watu kuwa biashara yako inaenda kufa, ndicho kitu cha ukweli.
Unaweza kuwaonyesha marafiki zako, ofisini kwako mambo yanaenda vizuri kabisa, kumbe nyuma ya pazia una changamoto nzito kweli kweli. Ambazo hujui kesho itakuwaje, ila kwa nje unaonyesha hakuna shida yeyote.
Unaweza kuwalaza watoto wako njaa, sio kwa sababu hakuna chakula, ila kwa sababu ya uzembe wako, wamelala njaa mara nyingi. Unawaabia hakuna kumwambia baba yenu kuwa hamkula, akiwauliza mwambieni mlikuwa mnaishi vizuri na kula vizuri.
Inawezekana kuna kundi unaliongoza, kundi ambalo limefika mahali linalalamikia mambo mbalimbali mabaya unayoyatenda. Kwa sababu una mamlaka, unawaziba midomo yao, kwa kuwaambia waseme kuna amani ya kutosha.
Unaweza ukawa unawatesa watoto uliowakuta wapo na mume wako, yaani wewe ni mama wa kambo. Ukawa unafanyia vituko vya ajabu ajabu, unawawekea kizuizi wasije wakasema kwa mume wako, wala ndugu yeyote. Unawatishia kuwafanyia jambo baya wakisema, kwa kuwa hawana pa kwenda, wanakuwa wanasema kuna amani ila mioyoni mwao wanalia kilio kikuu.
Haya mambo hayajaanza leo, wala usifikiri ni mambo mapya, wala usifikiri ni vitu vilivyoibuka hivi karibuni. Tangu zamani, haya mambo yalikuwepo, na Mungu alichukizwa mno na hilo, kusema kuna amani, wakati hakuna amani.
Rejea: Wameliponya jeraha la watu wangu juujuu, wakisema, Kuna amani, kuna amani, kumbe hakuna amani yoyote! Yeremia 8:11 BHN.
Nimeipenda Biblia ya habari njema, jinsi ilivyolitafuna hili andiko kwa kiswahili kilaini/chepesi kabisa. Unaona ni jinsi gani unaweza kuvalishwa vazi la amani, wakati hiyo amani huna kabisa.
Vizuri kutafuta suluhu ya jambo linaloondoa amani yenu/yako, kuliko kuendelea kudanganya watu amani ipo, kumbe hakuna amani yeyote.
Ukienda mbele za Mungu, jiweke wazi, mwambie Mungu sina amani kabisa, naomba unipe amani yako. Kama ndoa yako haina amani mweleze Mungu, kama ni familia yako haina amani mweleze Mungu, na kama ni kazi yako mweleze Mungu.
Usibaki na jambo lako kwa muda mrefu linalokuondolea amani yako, kufanya hivyo ni kujitafutia matatizo makubwa zaidi.
Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081