Utakuta kuna watu wanakuchokoza sana kwa maneno, kila ukijaribu kuwakwepa unakuta wapo na wewe tu, ukikaa kimya wanakuchokoza. Ukiwajibu maswali yao, wanakuuliza maswali mengine ya kichokozi(wengine husema maswali ya kizushi)
Unapokuwa mbele za watu unahutubia, au unahubiri, au unafundisha, wanakuwa wanakusikiliza kwa makini sana. Umakini huo sio kutaka kujifunza kupitia yale unazungumza, wanasubiri ukosee kuzungumza neno moja tu. Wapate sababu ya kukushtaki, sio kwamba ulilozungumza ndio limesukuma watu kukushtaki la hasha, ni chuki zao tu.
Watu wanaweza kukosa sababu kabisa ya kukuingiza hatiani kutokana na chuki zao binafsi, wakaanza kukutegeshea kwenye mazungumzo yako au kwenye kile unachopenda kufanya.
Kama unapenda sana kuandika, watakutegesha kwenye uandishi wako, kama unapenda sana kuimba, watakutegesha kwenye nyimbo zako, kama kazi yako ni udereva wa magari, kosa litatafutwa kwenye uendeshaji wako.
Unaweza kuona ni jinsi gani watu wenye chuki na wewe wakikudhamiria watakutafuta kila mahali, iwe kwenye serikali, au iwe kwa mtu binafsi, kama kuna cha kiMungu unachofanya. Na hicho kitu kinaharibu ngome za shetani, na kinamletea Mungu sifa na utukufu, uwe unajua upo mtegoni, siku ukitenda dhambi Dunia nzima itakuzomea.
Unaweza kujiuliza umefanya nini au umekosa nini hadi unatafutwa kiasi hicho, ukiwa mwaminifu mbele za Mungu, wewe ni mpinzani kwa mambo ya shetani. Unapokuwa mpinzani wa mambo mabaya, unakuwa adui wa shetani, huo uadui shetani anauweka kwenye mioyo ya watu wake, wanakuwa wanakutafutia visa.
Haya sio mambo mapya, ni mambo ambayo Yesu Kristo alikumbana nayo kwenye huduma yake. Unapoyaona yanakutokea wewe, hupaswi kushangaa sana.
Rejea: Alipotoka humo, waandishi na Mafarisayo walianza kumsonga vibaya, na kumchokoza kwa maswali mengi, wakimvizia, ili wapate neno litokalo kinywani mwake. LK. 11:53-54 SUV.
Sijui wewe unaviziwa kwa lipi katika maisha yako, unaweza kuwa unaviziwa uangukie dhambini, kama ni kaka unayemcha Mungu katika roho na kweli utategeshewa binti mzuri ili utembee naye kimapenzi wapate la kukushtaki. Kama ni dada, watakutegeshea wanaume wenye tabia mbaya ili ulale nao kimapenzi waweze kukushtaki.
Kama ni baba uliye mwaminifu mbele za Mungu na kwa mke wako, utategeshewa wanawake malaya ili utakapolala nao waweze kukushtaki. Na kukuondolea heshima yako mbele ya jamii na kuonekana hufai kuitwa mkristo safi.
Mitengo hii imewaangusha wengi sana hasa wale ambao hawakuwa makini, na hawakuta kumsikiliza Roho Mtakatifu. Lakini wewe ambaye unajifunza Neno la Mungu hupaswi kuingia kwenye mtego wowote mbaya, maana unakuwa makini kutokana na maarifa sahihi ya Neno la Mungu uliyonayo moyoni mwako.
Rejea: Wakamvizia-vizia, wakatuma wapelelezi waliojifanya kuwa watu wa haki, ili wamnase katika maneno yake, wapate kumtia katika enzi na mamlaka ya liwali. LK. 20:20 SUV.
Ndugu yangu, uwe macho sana, hasa wewe uliyeokoka, hasa wewe mwenye huduma, hasa wewe uliyetulia kwenye ndoa yako, hasa wewe unayesimamia haki ofisini kwako, hasa wewe unayependa kusimamia ukweli, hasa wewe unayependa kuusema ukweli.
Usianze kuishi kwa hofu, kwa sababu umeshajua haya, mshukuru Mungu kwa maarifa haya kupitia Neno lake, maana yatakusaidia kwenye maisha yako yote kwa kuwa karibu na Mungu zaidi. Pia elewa kwamba unalindwa na nguvu za Mungu, hakuna kilicho kinyume naye kitakachokudhuru maisha yako.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com
+255759808081