
Mtu yeyote akimpokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yake. Mtu huyo akajitoa kweli kwa Yesu, akawa hana mambo mengine machafu/mabaya.
Huyo mtu hatakuwa wa kawaida, kipo kitu ambacho kitakuwa tishio kwa Shetani.
Kitu chochote kinapokuwa tishio kwa Shetani, atatafuta kila njia kukuangusha au kukurudisha nyuma.
Wapo watu watakuja kutaka kujua siri ya mafanikio yako kiroho, unawezaje kuwa hivyo ulivyo, au unawezaje kutenda hayo.
Lengo lao sio kujifunza jambo la kuwasaidia katika maisha yao ya wokovu. Lengo lao ni kutafuta kukuangusha chini, ule uzuri wako ulio tishio kwa Shetani usiwe nao tena.
Hili tunajifunza kupitia maandiko, tunaona Samson alivyooa mwanamke wa Kifilisti. Huyo mwanamke alipewa kazi na wakuu ya kuhahakisha anajua siri za nguvu za mume wake.
Rejea: Nao wakuu wa Wafilisti wakamwendea, wakamwambia, Mbembeleze, upate kujua asili ya nguvu zake nyingi, na jinsi tutakavyoweza kumshinda, tupate kumfunga na kumtesa; nasi tutakupa kila mtu fedha elfu na mia moja. AMU. 16:5 SUV.
Mungu anaweza akawa anakutumia sana kwenye huduma yako aliyokupa. Usije ukajisahau, siku zote unapaswa kuwa makini.
Sio hilo tu, unapaswa kuwa na neno la Mungu la kutosha moyoni mwako. Hili litakusaidia kuzitambua hila za Shetani.
Sio hilo tu, Roho Mtakatifu anapaswa kuwa ndani yako, huyu ni kiongozi mzuri wa maisha yako.
Hakuna siku Shetani atafurahia vile unavyomharibia kazi zake, vile unavyowafanya watu wake wanazidi kumwamini Yesu Kristo.
Ndio maana unaweza ukaona mtumishi fulani alikuwa amesimama vizuri, baadaye unasikia ameanguka dhambini na maisha yake yamekuwa siyo.
Hiyo yote ni kazi ya adui, anahakikisha anapata kile kinakupa nguvu za kumsumbua yeye. Anaenda kukiharibu hicho hicho.
Usidharau hali yeyote unayoona kwako, ulikuwa mtu wa maombi lakini ghafla umeacha. Hiyo sio hali ya kufurahia kabisa.
Ulikuwa mtu wa kusoma sana neno la Mungu, lakini umefika mahali husomi tena. Hilo sio jambo la kupuuza, unapaswa kukataa hiyo hali.
Ulikuwa mtu wa kupenda sana mafundisho ya neno la Mungu, lakini ghafla hujisikii tena kupata mafundisho. Hiyo sio hali ya kufurahia kabisa.
Nguvu zetu za kiroho tulizonazo, na nguvu tunazozitumia katika huduma zetu. Usifikiri ni jambo la kumfurahisha kila mtu, hasa watenda kazi wa Shetani.
Kuepukana na hili ni kutoleta/kuepuka mazoea, unapaswa kuwa macho kiroho wakati wote.
Mungu akubariki sana.
Samson Ernest,
Mtenda kazi katika shamba la Bwana.
www.chapeotz.com
+255 759 80 80 81