Asifiwe Yesu, karibu sana tushirikishane machache ya kutujenga mioyo yetu katika safari hii ya wokovu.
Kuna mahali tunafika tunakuwa tumefungwa na mitazamo mbalimbali ya watu, juu ya changamoto tunazopitia katika maisha yetu.
Wakati mwingine tumekosa maneno ya kujitetea kutokana na kutojua Neno la Mungu vizuri, zaidi tumejikuta hatuna uwezo wa kusimama kwa miguu yetu kutoa hoja za kueleweka.
Wakati mwingine tumeonewa haki zetu kwa kushindwa kujitetea vizuri kutokana na kushindwa kwetu kupangalia maneno vizuri yakaeleweka.
Mtu anakuja kwako anakwambia utakuwa umemtenda Mungu dhambi ndio maana hujapata mtoto mpaka leo. Hivi kuna wanaume/wanawake wangapi ambao wanamtenda Mungu maovu kiasi kwamba huwezi hata kutazama uovu wao. Lakini wana watoto wengi tu.
Mwingine anaweza kukuambia mtoto wako au ndugu yako amekufa kwa sababu alikuwa mtenda dhambi sana, ni kweli Neno la Mungu linasema siku za mwenye haki zitaongezwa na siku za mwovu zinapunguzwa. Hivi kuna wenye dhambi wangapi unaowaona wanafanya uchafu kiasi kwamba unaona kama vile dunia imebaki siku mbili iteketezwe. Lakini bado wanaishi na wengine wamekuwa wazee sasa.
Rejea; Mbona waovu wanaishi, Na kuwa wazee, naam, na kuongezeka kuwa na nguvu? Kizazi chao kinathibitika nao machoni pao, Na wazao wao mbele ya macho yao. Ayubu 21 :7_8 SUV.
Mtu mwingine anaweza kutumia mwanya wa changamoto unayopitia kukuambia unateswa na mabaya, kwa sababu umepoteza uhusiano wako mzuri na Mungu. Wangapi wanafanya machafu na bado Mungu amewaacha na wanaishi vizuri kuliko hata wewe unayetunza utakatifu wako usije kumtende Mungu dhambi.
Rejea; Nyumba zao zi salama pasina hofu, Wala fimbo ya Mungu haiwapigi. Ayubu 21 :9 SUV.
Mwingine anaweza kukujia na kukuvuruga tu, kukuambia mbona biashara zako haziendi. Utakuwa huna Mungu aliye hai, wanakuonyesha za watu wa Mungu biashara zao zilivyostawi.
Wangapi ambao hawana habari na mambo ya wokovu na bado mambo yao yanaendelea vizuri.
Rejea; Fahali wao huvyaza wala hapungukiwi na nguvu; Ng’ombe wao mke huzaa, asiharibu mimba. Ayubu 21 :10 SUV.
Unapaswa kulijua Neno la Mungu vizuri, ili mtu asije akatumia mwanya wa andiko akakuangusha na kukupotezea mahusiano yako na Mungu. Ukiwa una uhakika hujapoteza uhusiano wako na Mungu, hupaswi kuyumbishwa na jambo lolote.
Shetani hana shida na mtu anayetenda mabaya wala hana shida na mtu asiyemzalia Mungu matunda. Shetani anakesha na mtu anayemcha Mungu katika roho na kweli na kumzalia Bwana matunda yaliyo mema.
Rejea; Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote. Zaburi 34:19 SUV.
Leo hii mtu anaanza kuhangaika na kukosa usingizi kisa ametabiriwa na Nabii fulani kuwa yeye ana mamikosi mengi. Anashindwa kujiuliza hiyo mikosi imetoka wapi na yeye ni mwana wa Mungu, anashindwa kuelewa hizo laana zimetoka wapi na wakati ameokoka. Kama zipo si angeenda mbele za Mungu kumwomba!
Wangapi hata hawamjui Mungu na wanaishi vizuri na hayo malaana hayawatesi, ukielewa vizuri haya mambo utabaki salama katika dunia ya iliyojaa uongo na utapeli mwingi.
Kweli kuna maeneo unajigundua ulikosea, ila yapo maeneo kabisa unaona hujamtenda Mungu dhambi. Alafu anakuja mtu anaanza kukuhangaisha na maneno magumu ya kukutisha, usikubaliana naye.
Mjue sana Mungu uweze kuhimili misukosuko mbalimbali ya maisha yako ya wokovu, ili ukikutana na jaribu ujue Mungu bado yu pamoja nawe na bado anakupenda.
Mungu akubariki sana mtu wa Mungu kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembeleaChapeo Ya Wokovukwa masomo mengine mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.