Ukiwa kama mzazi unaweza ukawa unatamani watoto wako au mtoto wako awe mtu fulani baadaye, kwahiyo malezi yako yanaweza yakawa yanamjengea uwezo mtoto wako aje awe mtu unayemtaka.

Siku zote unaweza ukawa unatumia muda wako mwingi sana kumjenga mtoto wako aje awe mtu fulani unayemtaka wewe. Sio kana kwamba unamtengeneza aje awe mtu fulani mbaya, la hasha unamtengeneza aje awe mtu mzuri kabisa.

Labda wewe ni daktari wa kutibu binadamu, unatamani mtoto wako aje awe daktari wa binadamu kama wewe ulivyokuwa, tena unatamani mtoto wako aje awe zaidi yako wewe.

Vile viwango vyako ulivyokuwa navyo, unatamani awe na viwango vya juu zaidi yako, ukiwa na mpango huo unaanza kumtafutia shule nzuri za viwango hivyo.

Labda wewe ni mchungaji, unatamani mtoto wako ashike mikoba yako ya utumishi, awe mtu ambaye maisha yake yote atayatoa kwenye eneo la kuchunga kanisa.

Unakuwa unatumia muda mrefu kukaa naye na kumwandaa vizuri kwa ajili ya kazi ya Mungu iliyo mbele yake, wakati mwingine unampa mazoezi kwa vitendo. Ili aanze kuzoea kwenye nafasi ambayo unataka awe.

Labda wewe ni mwimbaji wa nyimbo za injili, umekuwa mwimbaji kwa muda mrefu na huduma yako imezaa matunda mengi sana ndani na nje ya nchi. Umefika wakati unaona umri umeenda, unataka mtoto wako mmoja wapo ashike kijiti.

Pamoja na kutamani kote huko, pamoja na maandalizi yote hayo kwa mtoto au watoto wako, kama alivyofanya Samweli kwa watoto wake, waje wawe waamuzi au viongozi wa Israel.

Rejea: Hata Samweli alipokuwa mzee, aliwafanya wanawe wawe waamuzi juu ya Israeli. 1 SAM. 8:1 SUV.

Mambo yalikuwa tofauti kabisa na matarajio yake, ambapo hata kwa watu wengine wanaweza wakawa na wao walitegemea kitu kama hicho kutokana na utaratibu wao wa kipindi hicho.

Rejea: Ila wanawe hawakuenda katika njia zake, bali waliziacha, ili wapate faida; wakapokea rushwa, na kupotosha hukumu.1 SAM. 8:3 SUV.

Hii inatufundisha nini, inatufundisha kwamba matarajio yetu kwa watoto wetu kwa yale tunayotaka sisi wawe, yanaweza yakawa tofauti kabisa kama tulivyoona kwa watoto wa Samweli.

Yeye aliwaandaa waje wawe waamuzi juu ya Israel baada ya kuona yeye ameshakuwa mzee, akaandaa watoto watakao rithi nafasi yake. Badala yake watoto wale hawakuifuata ile njia waliyoelekezwa na baba yao.

Tuwaombee watoto wetu ila tusiwe na matarajio makubwa kwa kutumia nguvu zetu na akili zetu za kibinadamu bila kumtegemea Mungu afanye jambo juu ya watoto wetu.

Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
www.chapeotz.com
+255759808081