Hadi watu wakuamini na kutokuwa na wasiwasi na wewe, utakuwa umefanya kazi kubwa sana, tena utapaswa kuishi uhalisia wako.
Dunia ya sasa ilivyokaa, imani imetoweka sana, watu waaminifu wamekuwa adimu sana, upatikanaji wake umekuwa mgumu kwa watu hawa. Unaweza ukawa unatafuta mtu mwaminifu kwa haraka, huyo mtu ukamkosa kabisa.
Kumwona mtu anaaminiwa na watu, na kweli ukimchunguza ni mwaminifu kweli, huyo mtu ni wa kupongezwa sana na kutunzwa sana.
Ukitaka kujua Dunia ina uhaba wa watu waaminifu, ngoja nikupe mfano hai kabisa uliotokea siku chache zilizopita.
Kuna siku nilikuwa nimesafiri, wakati narudi nyumbani nilipanda gari aina ya Noah, wakati napanda sikutoa nauli na wala sikuambiwa niitoe. Naona nia yao ilikuwa waje wananidai wakati tumefika stand.
Muda ulipofika wa kushuka sasa, nilishukia njiani na kuondoka, sikuwa na kumbukumbu yeyote kama nilikuwa nimelipa au la. Sasa wakati naanza safari ya kurudi nyumbani baada ya kushuka kwenye gari, nikiwa kwenye tafakari zangu, nilikumbuka sikulipa nauli, nilijisikia vibaya sana kwa kitendo hicho.
Wakati natafakari nifanyaje, na nitampataje dereva wa Noah hiyo, wazo lilikuja kwamba niende stand nikaulize gari lililoingia muda huo kutoka mahali fulani imepakiwa wapi (kumbuka mimi sikushukia stand ndani)
Nilivyoingia stand humo, na giza lilishaanza kuingia, maana ilikuwa ni jioni, niliuliza na kuonyeshwa mahali limepaki hilo gari aina ya Noah. Nilivyomwangalia dereva, na wakati tunaendelea na safari alikuwa amefungulia radio, moja kwa moja nilijua ni lenyewe.
Baada ya kufika na kuona hivyo viashiria, nilimuulize hili ndio gari la kutoka mahali fulani? Akanijibu ndio, nikamwambia nilisahau kulipa nauli yangu, nimekumbuka njiani wakati naelekea nyumbani. Nikawapa nauli yao.
Walikuwa na mwenzake hapo wanaongea, walishangaa na kusema kaka utakuwa umeokoka wewe… na kuongea maneno mengi ya mshangao!
Furaha yao ya mshangao ilimfanya huyu dereva na mwenzake watoe Noah yao stand, wanisindikize mahali naenda ambapo ilikuwa nyumbani.
Kwanini nakueleza haya, ni kukuonyesha kiasi gani watu waaminifu wanazidi kuwa adimu ndio maana inaonekana ni jambo lisilowezekana, kupitia mfano huu halisi kabisa, inaonyesha watu wamekosa uaminifu kwa wenzao.
Haya yote yamekuja kwenye tafakari yangu, baada ya kuona hata Yesu Kristo mwenyewe, watu walimwamini kwa ishara zake alizofanya.
Rejea: Hata alipokuwapo Yerusalemu kwenye sikukuu wakati wa Pasaka, watu wengi waliamini jina lake, walipoziona ishara zake alizozifanya. YN. 2:23 SUV.
Ndivyo ilivyo hata kwetu, ili watu watuamini, lazima kuna ishara tunapaswa kuzionyeshe kwa watu hao, hatutakaa tuaminiwe ipasavyo kama hatutaonyesha ishara fulani za uaminifu.
Ndio maana nilisema mwanzo mpaka watu wakuamini utakuwa umefanya kazi kubwa sana, maisha yako hayapaswi kuwa ya kuigiza, ukiigiza maisha yako. Itafika mahali watu watakugundua tu, na watapokugundua, hawatakaa wakuamini tena.
Watu kuliamini jina la Yesu Kristo, haikuwa hivi hivi, Yesu Kristo alifanya kazi kweli kweli, waliona ishara zake kubwa alizofanya kwa watu, ndipo wakamwamini Yesu Kristo.
Nawe jitahidi kuishi maisha matakatifu na yaliyojaa uaminifu mkubwa, usipoaminiwa na watu, utapata tabu sana kwa Dunia ya sasa.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest
www.chapeotz.com