Sio jambo geni kwetu pale unapomwomba ndugu yako, au rafiki yako, au jirani yako msaada wake. Anakaa kimya bila kukupa ushirikiano wowote.

Baadaye unaamua kumtazama Mungu wako, hitaji lako ulilokosa msaada kwa wale uliowategemea wakusaidie katika jambo fulani. Unaamua kurudi kwa Yesu mwenyewe akusaidie juu ya hitaji lako.

Kwa kuwa Yesu Kristo ni mwaminifu kwa wale wamchao katika roho na kweli, anakusaidia, anakuinulia watu ambao hukuwategemea kama wangetokea kukusaidia.

Sio watu tu, anakupa uwezo au mawazo, au ujasiri, au nguvu za kuweza kulitenda lile ambalo uliomba msaada ukaukosa kabisa.

Baadaye Mungu anakusaidia, ama anakufanikisha lile ulikuwa unahitaji, wale wale uliwaomba msaada wao. Wanarudi kukulaumu kwanini umefanya mambo yako kimyakimya bila kuwashirikisha wao.

Tena sio kukulaumu tu, wanakupa na matisho yao, wanasahau siku uliwaomba msaada wao na wakakaa kimya, au wakatoa sababu ya kutoshirikiana na wewe.

Hili halijaanzia kwako au kwetu, tunaona kupitia maandiko ya Biblia Takatifu, Yeftha alikumbwa na hili jambo, au na hichi kisa nilichoanza kukueleza hapo mwanzo.

Rejea: Kisha watu wa Efraimu walikutana pamoja na kupita kwenda upande wa kaskazini; wakamwambia Yeftha, Kwa nini wewe kuvuka kwenda kupigana na wana wa Amoni, nawe hukutuita sisi kwenda pamoja nawe? Tutaipiga moto nyumba yako juu yako. AMU. 12:1 SUV.

Ukisoma huo mstari kwa umakini, utajifunza mambo mengi sana ambayo yatakusaidia kuelewa hili ninalokueleza hapa.

Uzuri ni kwamba mtu unapoamua kuachana na wale uliowaomba msaada wakaa kimya au wakakuambia hawawezi kukusaidia. Unakuwa na majibu ya kuwajibu kabisa, huwezi kukosa majibu yake.

Yeftha anatudhihirishia hili, akawapa jibu sahihi, kile ambacho kilimfanya achukue hatua ya kwenda kufanya bila kushirikiana pamoja nao.

Rejea: Yeftha akawaambia, Mimi na watu wangu tulikuwa na matata makubwa na wana wa Amoni; nami hapo nilipowaita ninyi, hamkuniokoa na mikono yao. Nami nilipoona ya kuwa ninyi hamniokoi, niliuhatirisha uhai wangu, na kuvuka ili nipigane na wana wa Amoni, BWANA naye akawatia mkononi mwangu; basi kwa nini ninyi kunijia hivi leo kutaka kupigana nami? AMU. 12:2‭-‬3 SUV.

Kuna wakati mwingine inabidi uhatarishe maisha yako mwenyewe, ikiwa Mungu yupo upande wako atakupigania na vita hivyo utavishinda.

Ndicho kilichotokea kwa Yeftha, alivyojitoa mwenyewe Bwana hakumwacha peke yake, wale maadui zake walitiwa mikononi mwake. Na vita vile alivishinda.

Hichi kisa kinatufunza mambo mengi sana ya muhimu katika maisha yetu ya kila siku, maana mambo kama haya tunakutana nayo.

Tunapokutana nayo hayawezi kutushtua sana maana tayari tunayo maarifa sahihi ya neno la Mungu. Hii inasaidia kupata ujasiri wa kuendelea mbele pasipo kuyumbishwa na jambo lolote, au na hali yeyote.

Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
Mtenda kazi katika shamba la Bwana.
www.chapeotz.com
+255 759 80 80 81.