Mara nyingi mtu akibananishwa na shida ngumu anaweza kuomba msaada kwa unyenyekevu sana.

Anaposaidiwa kile ambacho alikuwa anataka asaidiwe, huwa anasahau na kurudi kwenye hali yake ile ile ya mwanzo.

Hali ambayo ilimsababishia akaingia kwenye shida ngumu, shida ambayo asingeweza kuondokana nayo hadi asaidiwe.

Mtu anaomba msamaha kweli wakati amebebanishwa kwenye shida, anaahidi atorudia tena kosa. Lakini baada ya kumpa msaada mwingine anakubadilikia.

Labda ulikuwa umemkopesha kiasi fulani cha fedha, kile ambacho ulikuwa unamdai alikuwa hataki kukurudishia.

Sio hataki tu kukurudishia, alifika kipindi akasema hujawahi kumpokesha kabisa.

Baadaye akabanwa kisawasawa na matatizo ya Dunia hii, anakuja kulia shida sana kwako. Anaahidi vitu vingi na kusema atakulipa pesa zote unazomdai.

Baada ya kumsaidia tu kuzungushwa kunarudi pale pale. Unaanza kujuta kwanini ulimsaidia na anajua alikuwa ni mtu ambaye ni msumbufu.

Hujamaliza hilo na kusema umekoma, anarudi siku nyingine kwa njia tofauti ya kutia huruma sana.

Ukiangalia kweli unaona msaada wako ni muhimu sana kwake, na moyoni mwako unasukumwa kufanya hivyo.

Watu kama hawa leo tutawaita akina Farao katika somo hili, utajiuliza ni kwanini? Twende pamoja utanielewa vizuri.

Rejea: Ndipo Farao akawaita Musa na Haruni na kuwaambia, Mwombeni BWANA, ili awaondoe vyura hawa kwangu mimi na kwa watu wangu; nami nitawapa watu ruhusa waende zao, ili wamtolee BWANA dhabihu. KUT. 8:8 SUV.

Ukisoma habari ya Farao aliyekuwa anawazuia na kuwatesa wana wa Israel wasiende kumtolea Mungu wao dhabihu.

Mungu alipotoa mapigo kwake, aliwaomba Musa na Haruni wamwambie Mungu asitishe mapigo yale.

Alichowahidi ni kwamba atawaruhusu waende wakamtolee Mungu wao dhabihu.

Lakini baada ya Musa kumwomba Mungu asitishe pigo alilotoa, Farao alirudi kwenye hali yake ile ile ya mwanzo.

Rejea: Lakini Farao alipoona ya kuwa pana nafuu, akaufanya moyo wake kuwa mzito, asiwasikize; kama BWANA alivyonena. KUT. 8:15 SUV.

Tunao akina Farao katika maisha yetu ya kila siku, watu ambao wanatubu leo na kukiri kutorudia kosa ila ukishamsaidia anarudia yale yale ya mwanzo.

Ukiwa kwenye kundi hili la akina Farao wa leo, vizuri kuachana na hiyo tabia. Usipoacha utashindwa kusaidiwa na watu, maana watakuwa wanakuogopa.

Mungu atusaidie sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com