Kuna msemo unasema hivi, kilio cha wengi ni furaha, msemo huu huwafariji wengi hasa wanapojikuta wote wapo katika tatizo moja.

Mtu anajisikia faraja zaidi pale anapoona shida anayopitia/iliyompata wapo wengi zaidi wanapita jambo lile. Au mwingine anajisikia faraja pale anapoona linalomsumbua yeye wapo wengine wengi zaidi wanasumbuliwa na tatizo kama lake.

Mtu anaweza kujisikia amani pale anapotenda dhambi, akaona kundi kubwa la watu na wao wanatenda dhambi. Anaona anachokifanya yeye, hayupo peke yake, wapo wengine wengi zaidi wanafanya uchafu kama wake.

Ndio maana ukiwa katika makundi, yanaweza kuwa makundi ya shuleni/chuo, au kambi yeyote ile. Ukionekane huendi pamoja na wenzako katika starehe mbalimbali za dunia, unaonekana mshamba. Ndio maana wengi huwa wanabadilika wakifika chuo, ile misimamo yao ya kutomtenda dhambi huwa inayeyuka ili wasionekane hawajui kitu.

Kufuata mkumbo wa wengi wanaofanya mabaya, haiwezi kukufanya uepukane na ghadhabu ya Mungu juu yako. Usifikiri mkiwa wengi katika kutenda dhambi ndio itakuwa pona yako au itakuwa ahueni kwako.

Hukumu ya Mungu inaposhuka/itakapoachiliwa, haitaangalia mlikuwa wote, katikati ya wote, wapo watu walikuwa wanajitenga na maovu. Wapo watu walikuwa wanamlilia Mungu wao usiku na mchana kuhusu uovu mliokuwa mnaufanya.

Hakuna kisingizio cha kuja kusema nilimwona fulani anafanya mabaya nikaona na mimi nifanye. Siku ya hukumu ya Mungu, atabagua walio wake, haijalishi watakuwa wawili katikati ya mamilioni ya watu. Hao hao Mungu atawathamini na uchache wao.

Kwa Mungu hakuna kilio cha wengi, ukisema mbona wengi wanafanya dhambi ngoja na mimi nifanye. Uwe na uhakika wapo ambao hawatakubali kumtenda Mungu wao dhambi, hata kama wote mtaona fasheni kumtenda Mungu dhambi.

Utasema kanisa lote hili la watu wengi hivi, lenye mamilioni ya watu, Mungu hawezi kuliangamiza kabisa. Kwa kutazama wingi wa watu unaona Mungu hawezi kuliangamiza kanisa lote hilo, utasema Mungu hawezi kuliangamiza taifa lote hili.

Upo sawa kabisa kusema Mungu ni mwenye upendo, Mungu ni mwenye huruma, hawezi kabisa kuwaangamiza. Kama mnaabudu sanamu, kama mnaabudu miungu mingine, kama mnatenda maovu, amini Mungu hatakuhurumia kwa hayo kama hautaokoka.

Usiangalie wingi wa watu wanaomtenda Mungu dhambi, ukafikiri Mungu atawaacha, unaweza kujidanganya vyovyote vile. Unaweza kujifariji vyovyote vile ila kumbuka Mungu haangalii kama wewe uangaliavyo.

Usitoe sababu kwa kuangalia wingi wa watu, kila mmoja atahukumiwa sawa sawa na matendo yake. Hakuna cha kilio cha wengi ni furaha, hakuna furaha kwenye ziwa la moto.

Hili liliwakuta wana wa Israel, kabla Mungu hajaachilia pigo lake la maangamizo, alitoa agizo la wale watenda mema wote wawekewe alama kwenye vipaji vya nyuso zao. Ili Mungu atapoachilia pigo lake, wasiweze kudhurika na chochote.

Rejea: BWANA akamwambia, Pita kati ya mji, kati ya Yerusalemu, ukatie alama katika vipaji vya nyuso vya watu wanaougua na kulia kwa sababu ya machukizo yote yanayofanyika kati yake. EZE. 9:4 SUV.

Umeona hapo? Unaweza kurudia tena kusoma hilo andiko, utaona Mungu alivyotoa agizo lake kwa wale waliokuwa wanaugua na kulia kwa ajili ya machukizo yaliyokuwa yakifanyika(hawa ni wacha Mungu).

Acha marafiki zako wote watende dhambi, acha ndugu zako wote waache wokovu, acha watu wako wote wa karibu unaowaamini sana warudi nyuma. Wewe usikubali kuwafuata, endelea kuishi maisha ya kumpendeza Mungu wako.

Mungu anakuona, Mungu atashusha ghadhabu yake juu ya nchi yako ila wewe utapona, ndio utapona, amini hivyo. Usije ukasema bora na mimi kuwafuatisha marafiki zangu, kama ni moto huo tutaingia wengi, kumbuka hakuna maumivu/mateso ya kuchangia.

Tena Mungu alisisitiza wauliwe watu wote, bila kujalisha Umri wao, isipokuwa wasiguswe wale alioagiza wawekewe alama kwenye VIPAJI vya nyuso zao.

Rejea: Waueni kabisa, mzee, na kijana, na msichana, na watoto wachanga, na wanawake; lakini msimkaribie mtu ye yote mwenye hiyo alama; tena anzeni katika patakatifu pangu. Basi, wakaanza kwa wazee waliokuwa mbele ya nyumba. EZE. 9:6 SUV.

Kama ulikuwa hujui madhara ya kufanya dhambi kwa kuangalia wingi wa watu, jifunze kuanzia leo, acha kabisa kufuata mkumbo. Ishi maisha ya kumpendeza Mungu, acha kuabudu sanamu, acha kuabudu miungu mingine, nasema acha kabisa. Maana kilichowapelekea hawa kutekezwa na ghadhabu ya Mungu ni hayo.

Kama ulikuwa unatunza maisha yako ya wokovu, kama ulikuwa unatunza utakatifu wako, na kama ulikuwa unajilinda na uovu. Endelea hivyo hivyo, Mungu anakuona sana, hawezi kuangamiza chochote bila kuweka alama yake kwako.

Mungu akubariki sana.
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.