Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, habari za muda huu ndugu katika Kristo.

Tupo tayari kusikiliza ila hatupo tayari kusikia ukweli, tupo tayari kuambiwa mambo yalivyo kuwa ila hatupo tayari kuambiwa jambo linalogusa maisha yetu vibaya.

Uwe na uhakika unayeenda kumpa ukweli, awe tayari kweli kuupokea huo ukweli, yupo tayari mtu kuambiwa hutokufa na wakati atakufa. Hata sijui kama unanielewa hapa, umewahi kupewa taarifa ya kifo alafu ukawa unaomba kimoyomoyo isije ikawa taarifa ile ni ya kweli.

Umewahi kwenda kupima ugonjwa ambao ni hatari kwa afya yako kama utakutwa unao huo ugonjwa, na ukawa na uhakika kwa vyovyote vile unaweza kuwa nao maana njia zako hazikuwa vizuri. Pamoja na kwenda kwa dokta kupima, moyoni mwako unaona kabisa huna hata chembe ya kuupokea ukweli wenye taarifa ya kuumwa kwako. Ila upo tayari kupewa majibu mazuri yenye kuufurahisha moyo wako, na si ukweli wenyewe.

Labda nikupe mfano huu unaweza ukanielewa zaidi, mdada amelala na mwanaume kwa uasherati alafu baada ya muda akaanza kusikia hali fulani isiyo ya kawaida. Anaenda kupima mimba ili kujihakikishia zaidi ila ndani ya moyo wake anajua kabisa kwa mchezo aliocheza lazima atakuwa nayo, ila dada yule hayupo tayari kupokea majibu ya kuambiwa anayo mimba pamoja na ameenda kupima.

Mungu akupe hekima katika hili la kuutoa ukweli, ndio maana unaona nesi aliyefunzu mafunzo vizuri. Hawezi kukupa majibu ya HIV kwa haraka, lazima akupitishe maeneo mbalimbali ya kukujenga kifikra usije ukapoteza uhai wako kwa taarifa utakayopewa.

Wengi wetu wanatamani kuijua kweli ya Mungu, ila hawapo tayari kuambiwa ukweli wa Neno la Mungu, yaani kwa maana nyingine ndani mwao kuna mipaka ya kupokea vitu. Haijalishi wana kiu kiasi gani ya kumjua Mungu, ndani mwao wanaweza kukataa kabisa ukweli, na huwezi kumlazimisha kwa hilo mtakosana.

Hili tunaliona kwa Mikaya, alikuwa ni msema kweli wa Mungu, ni moja wa manabii ambao walisema ukweli wa Mungu. Ila kutokana na mfalme wa Israel kutopenda kuambiwa ukweli, ilimpelekea kumchukia sana Mikaya japo alihitaji msaada wake.

REJEA; Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Yupo mtu mmoja, ambaye tungeweza kumwuliza BWANA kwa yeye; lakini namchukia; kwa sababu hanibashirii mema kamwe, ila siku zote mabaya; naye ndiye Mikaya mwana wa Imla. Yehoshafati akasema, La! Mfalme asiseme hivi. 2 NYA. 18:7 SUV.

Ukisoma zaidi hii sura unaona Mikaya aliamua kupindisha ukweli, kutokana na kumfahamu mfalme hapendi ukweli. Ili ajiepushe na mikono ya mfalme, ila baadaye tunaona alivyonyoosha ukweli, ilimpekelea kufungwa gerezani.

REJEA; Mfalme wa Israeli akasema, Mchukueni Mikaya mkamrudishe kwa Amoni mkuu wa mji, na kwa Yoashi mwana wa mfalme; mkaseme, Mfalme asema hivi, Mtieni huyu gerezani, mkamlishe chakula cha shida, na maji ya shida, hata nitakaporudi kwa amani. 2 NYA. 18:25‭-‬26 SUV.

Elewa haya ndugu yangu, itakusaidia sana maeneo mengi katika maisha yako, sikuambii uwe unanyamaza kwa vitu unavyoona usiposema utaulizwa na Mungu. Tumia akili na hekima iliyo ndani yako kuyanena yale Mungu amekusukuma uyasema, huku ukijua muda wowote linaweza kutokea la kutokea kama Mikaya.

Kung’ang’ania kwa mtu umwambie ukweli, sio mara zote yupo tayari kuupokea ukweli, wengine wanahitaji maneno mazuri yasiyoumiza mioyo yao. Hata kama unachowaambia sio kweli, ilimradi maneno yale yanamtetea yeye aendelee kuwa juu.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
Chapeo@chapeotz.com