Kuna wakati utafika itabidi umsifu Mungu wako kwa matendo yake makuu katika maisha yako, baada ya kupita kwenye nyakati ngumu katika maisha yako. Nyakati ambazo hukuwa na uhuru wa kumtumikia Mungu wako.

Zipo changamoto ngumu ambazo mtu anakuwa nazo, changamoto ambazo zinakuwa sehemu ya maumivu kwake, hata ile hamu ya kufanya mambo ya Mungu inakuwa chini sana.

Wengine hufika mahali wakaanza kumlaumu Mungu, wanaona kama vile Mungu wameawaacha, hawana tena msaada wa kuwasaidia kuvuka eneo ngumu walilokuwa wanapitia.

Wengine hufika mahali hawaoni ndugu wa kuwatia moyo katika shida, mtu alikuwa anaumwa anafika mahali ambapo haoni ushirikiano wa ndugu zake tena.

Lakini pamoja na hayo yote, itafika saa ya huyu mtu kumwona Mungu akimponya na ugonjwa wake, akimvusha kwenye jaribu zito alilokuwepo.

Baada ya kuvushwa kwenye magumu aliyokuwa anapitia, mtu huyo lazima awe na wimbo ndani yake, wimbo wa kumtukuza Mungu kwa matendo yake makuu katika maisha yake.

Haijalishi mtu huyo hujawahi kumwona akiimba kwaya yeyote ile, haijalishi mtu huyo hana sauti nzuri sana ya kuvutia wengine katika uimbaji wake. Uwe na uhakika wimbo atakaouimba unaweza kubadilisha maisha ya watu wengine, maana anao wimbo wa ushuhuda wake.

Rejea: BWANA ni nguvu zangu, na wimbo wangu; Naye amekuwa wokovu wangu. Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu; Ni Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza. KUT. 15:2 SUV.

Huyu ni Musa akimwimbia Mungu baada ya kuwatoa Misri na kuwavusha bahari ya shamu, baada ya kushuhudia farasi, magari, na jeshi lote kumezwa na maji.

Rejea: Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini, Maakida yake wateule wamezama katika bahari ya Shamu. Vilindi vimewafunikiza, Walizama vilindini kama jiwe. KUT. 15:4‭-‬5 SUV.

Pale unapofika mahali unamwona Mungu akiwashughulikia maadui zako, akishughulika na ugonjwa wako, akishughulika na mume/mke wako, akishughulika na familia yako, na akishughulika na kila aina ya shida yako.

Rejea: BWANA, katika miungu ni nani aliye kama wewe? Ni nani aliye kama wewe, mtukufu katika utakatifu, Mwenye kuogopwa katika sifa zako, mfanya maajabu? KUT. 15:11 SUV.

Nataka ufahamu kwamba kila mtu aliye kwa Yesu Kristo, aliyeshikamana sawasawa na Yesu Kristo, ana siku yake ya kumwimbia Bwana wimbo wake wa sifa.

Haijalishi unapitia kwenye changamoto gani, endelea kushikamana na Yesu Kristo, ipo siku yako ya kumwimbia wimbo wa shukrani, wimbo unaotoka ndani ya vilindi vya moyo wako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081