Kuwa upande wa Mungu ni bora zaidi, kuliko kuwa upande ulio kinyume na Mungu wako. Kuwa upande ulio kinyume na Mungu, ni kujitafutia matatizo mabaya kwenye maisha yako ya kiroho na kimwili.

Matendo mabaya ni kwenda kinyume na Mungu wako, unapofanya dhambi, yaani unapotenda yale matendo maovu mbele za Mungu. Moja kwa moja unafarakana na Mungu wako, Mungu anapokuambia usiabudu miungu mingine, wewe ukaabudu. Huko ni kwenda kinyume na agizo la Mungu.

Mungu anapokuambia usiabudu sanamu ya aina yeyote ile, alafu wewe ukaenda kuinyenyekea sanamu iliyochongwa kwa kuiabudu. Huko ni kwenda kinyume na maandiko matakatifu, huko ni kumkasirisha Mungu wako, huko ni kujitafutia matatizo mbele za Mungu.

Tena wale wote wanaoshirikiana na wewe kukupa nguvu za kuendelea kuabudu miungu yako, wale wote wanaokuunga mkono kuabudu kwako sanamu. Adhabu yenu ni moja mbele za Mungu, hata kama hawajionyeshi moja kwa moja mbele za watu kukuunga mkono.

Wengine wanawezaje kuhusika? Wanaweza kuhusika kwa michango yao mbalimbali kuhakikisha unajenga mahekalu ya kuabudu miungu/sanamu. Hawa wawezeshaji wanaoweza kukusaidia kuendelea kueneza yale yaliyomachukizo mbele za Mungu, hukumu yenu ni moja.

Labda nikupe mfano huu rahisi, ili uweze kunielewa vizuri, kama kuna adui yako anakusumbua sana. Huyo adui yako akawa ana watu nyuma yake wanaompa ushirikiano wa kuendelea kukusumbua. Uwe na uhakika kama umesimama na Mungu wako vizuri, siku Mungu anashusha adhabu yake kwa adui yako, adhabu hiyo itawahusu na wale wote waliokuwa wanashirikiana na aliyekuwa anakusumbua.

Hivi ndivyo ilivyotokea Misri, wale wote waliokuwa wanamsaidia Misri, hukumu ya Mungu iliwapata na wao. Inaweza kuwa kwa hali ya kawaida hakuwa wakionekana sana wakitoa ushirikiano kwa Misri, japo Misri wenyewe walikuwa wanajua ila wale wasio wa Misri huenda iliwawia ngumu kuelewa hayo.

Rejea: BWANA asema hivi; Nao pia wanaoitegemeza Misri wataanguka, na kiburi cha uwezo wake kitashuka; toka Migdoli hata Sewene, wataanguka ndani yake kwa upanga, asema Bwana MUNGU. Nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapoweka moto katika Misri, na hao wote wamsaidiao watakapoangamia. EZE. 30:6‭, ‬8 SUV.

Hapa tunapata kujua pia adui yako wakati mwingine hawezi kuwa na nguvu zake za kujitegemea mwenyewe. Wakati mwingine nguvu za adui yako zinachangiwa na kundi kubwa lililo nyuma ya huyo anayekusumbua.

Misri haikuwa peke yake, kuna marafiki zake waliokuwa wameungana na Misri katika kumsaidia. Msaada wa kumsaidia Misri, ukasababisha maangamizo ya Mungu yawapate na wao wasaidiaji.

Mungu atusaidie sana.
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.