Haleluya,
Tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kutupa wokovu bure, kwa gharama kubwa aliyeitoa YESU Kristo MSALABANI.
Tunajua wote wanawake walivyo na huruma na uchungu na watoto wao, ila sio kweli wanakuwa na huruma ile tunayoisema sisi.
Unaweza kusema kwanini unasema hivyo, nasema hivyo kwa sababu hii;
Mara ngapi wamama/wadada wanatoa mimba zao? Tena wengine mimba zao zilishakuwa kubwa kabisa.
Mara ngapi wamama/wadada wanazaa watoto lakini wanawatupa chooni? Ni wengi sana na wakati mwingine watoto wamefia humo bila kujulikana kwa wengine.
Mara ngapi wamama/wadada wametupa watoto kwenye majalala ya takataka huku wamewafunga kwenye mifuko ya lailoni? Bila shaka tumeshuhudia mara nyingi sana hili.
Hapo ipo huruma gani, hapo ipo hofu gani, hapo upo upendo gani, hayo yote utasema hawana hofu ya Mungu. Kama ni hivyo si inajulikana kuwa uchungu wa mwana aujue mzazi? Sasa ule uchungu wa kuzaa na kubeba mimba miezi tisa upo wapi?
Ikiwa mama yako aliweza kukutupia kwenye shimo la choo, ukaokolewa na wasamaria wema. Iweje leo mume/mke wako ashindwe kukugeuka? Inawezekana kabisa.
Ikiwa dada/mama ulipata ujasiri wa kutoa mimba au ulipata ujasiri wa kumtupa yule mwanao. Itashindikana vipi mchumba/mume wako kukubadilikia na kukuambia sikutambui?
Unaweza kusema ndugu acha kunidanganya, mama hawezi kumwacha mwanaye aliyemzaa kwa tumbo lake. Nisiwe mbishi kwa hili, niombe nikupe hili andiko.
Rejea; Baba yangu na mama yangu wameniacha, Bali BWANA atanikaribisha kwake. ZAB 27:10 SUV.
Umeona hapo tena huu mstari umepewa nguvu zaidi tukisoma katika kitabu cha Isaya 49:15, inasema hivi; Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe. ISAYA 49:15 SUV.
Kwanini usitoe maisha yako kwa asilimia 100, sehemu unayoona haiwezekani kuachwa ukiwa mwaminifu kwake. Hata ukikosea unaweza omba toba ukasamewa, na maisha yakaendelea.
Haijalishi utajikuta upo katika nyakati gani za kutengwa na ulimwengu mzima, ila Maandiko yanasema hivi;
Umngoje BWANA, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje BWANA. ZAB. 27:14 SUV.
Mkimbilie Bwana ndugu yangu, hata kama unaona hali ni shwari. Unapaswa kujitoa kwa Bwana haswa maana yeye ndiye anayetuokoa na tabu zote.
Rejea: BWANA ni nguvu zangu na ngao yangu. Moyo wangu umemtumaini, Nami nimesaidiwa; Basi, moyo wangu unashangilia, Na kwa wimbo wangu nitamshukuru. ZAB. 28:7 SUV.
Nakukumbusha tena na tena, mwanadamu anaweza kuonekana ana upendo sana kwako ukafika hatua ukahitaji msaada wake akashindwa kukusaidia.
Unaweza kutenda yote mema kwa mtu, ila ikafika siku akasahau wema wote uliowahi kumtendea. Na akageuka kuwa mwiba/machungu kwako, akageuka jeraha kwako, akageuka gereza kwako.
Mtegemee Mungu siku zote za maisha yako, leo baba yako na mama yako wanakupenda, ipo siku hautakuwa nao. Leo dada unapendwa na wazazi wako, ila siku umepata mimba isiyo na ndoa, watakufukuza kama mbwa. Lakini Mungu hawezi kukuacha kamwe.
Mshike sana Yesu Kristo, mimi leo naweza kuwa rafiki yako ila kesho ukawa adui yangu. Leo unaweza kusema nina ndugu wa kutosha, ikafika siku hao ndugu usimwone akikusaidia hata mmoja.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.