Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, habari za muda huu ndugu yangu, wakati mwingine tena wa kwenda kukushirikisha tafakari hii mhimu sana.

Zipo nyakati zinaweza kutufanya tukawa njia panda, yaani tukashindwa tuchukue uamzi gani katika jambo fulani linalotuweka njia panda. Tunapofika nyakati kama hizi huwa tunaanza kutafuta watu wa kutusaidia mawazo mema, ya kutusaidia tuweze kuchukua hatua sahihi.

Wengi wetu tunakuwa tayari tunajua wapo watu ambao hatupo tayari kuufuata ushauri wao, na tunajua kabisa wapo watu tunaweza kufuata ushauri wao. Hata kama hawa watu watatupa ushauri usiofaa, kwa kuwa tayari tumejiwekea utayari wa kupokea kile wanatuambia, huwa tunaufuata ushauri wao.

Mara nyingi watu tunaowapuuza ni wale wanaotuzidi umri, na kuona watu wanaoweza kutupa ushauri mzuri zaidi ni vijana wenzetu wa rika letu. Tunasahau wazee wetu ndio wenye busara zao, ambazo wao huwa hawaendani sana na mihemko ya ujana maana walishapitia hayo wanajua.

Kundi lingine ni wale wanaotuzidi umri naamanisha sio wazee, tunakuwa na jambo ambalo linatuzidi akili. Tunapoenda kwao kuomba ushauri, tunakuwa tunaenda tu ila hatupo tayari kuufanyia kazi ushauri wao. Ila tunataka tu kuonekana tuliomba ushauri kwao.

Tunajua sio kila ushauri unaweza kuubeba na kuufanyia kazi, ushauri mwingine ni wa kusikiliza na kuachana nao. Maana ukiangalia matokeo ya ushauri ule ukichukua hatua, unaona kabisa kuna madhara makubwa mbeleni yatatokea kwa kuufanyia kazi ushauri ule.

Hapa ninachokizungumza ni ule ushauri mzuri unaoupata kwa watu unaoheshimiana nao, kuhusu lile ulioenda kuwaomba ushauri. Japo sio kila unayeheshimiana naye anaweza kukupa ushauri mzuri, wengine wanaweza kukupa ushauri wa kukuangamiza. Ndio maana nikakuambia uwe mwangalifu kwa hili, isije ikakuletea majuto baadaye.

Labda umeenda kuomba ushauri kuhusu mtu aliyekukosea kosa ambalo linakuumiza moyo wako sana, badala ya kupewa ushauri wa kuweza kumalizana na hilo jambo kwa wema. Unapewa ushauri wa kulipiza kisasi juu ya yule aliyekukosea, hapo unaweza kuona huo ushauri sio wa kufuata.

Tunamwona kiongozi mmoja hapa kwenye biblia, akienda kuomba ushauri wa wazee, akapewa ushauri mzuri wa namna ya kukabiliana na hilo aliloenda kuomba kushauriwa. Lakini hakuridhika na ushauri ule, ikabidi aende kuomba ushauri kwa vijana, ambapo vijana wale walimshauri vibaya.

Rejea: Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee, waliosimama mbele ya Sulemani baba yake, alipokuwa hai bado, akasema, Mwanipa shauri gani la kuwajibu watu hawa? Wakamwambia, wakasema, Ukiwa mwema kwao watu hawa, na kuwapendeza, na kuwaambia maneno mazuri, ndipo watakapokuwa watumishi wako siku zote. 2 NYA. 10:6‭-‬7 SUV.

Huo ni ushauri wa wazee waliomshauri namna ya kuishi na watu wale, walimpa njia nzuri sana ya kuenda pamoja na watu wale. Lakini hapa tunaona akigeuka njiani ya pili kwenda kwa vijana kumshauri awafanye nini watu wale.

Rejea: Lakini akaliacha shauri lile la wazee walilompa, akataka shauri kwa wale vijana waliokua pamoja naye, waliosimama mbele yake. Akawaambia, Je! Mwanipa shauri gani la kuwajibu watu hawa, waliosema nami, wakisema, Utufanyie jepesi kongwa alilotutwika baba yako. Na wale vijana waliokua pamoja naye wakamwambia, wakasema, Uwaambie hivi watu wale waliosema nawe, wakinena, Baba yako alilifanya zito kongwa letu, lakini wewe tufanyie jepesi; uwaambie hivi, Kidole changu cha mwisho ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu. 2 NYA. 10:8‭-‬10 SUV.

Umeona hapo, akauacha ushauri mzuri akautafuta ushauri mwingine mbaya, ambao kwa yeye aliona ungemfaa sana. Na kweli aliona ushauri wa vijana wale ni bora sana kuliko wa wazee, kumbe ubora ule ulikuwa sio ubora.

Tunaweza kuona zaidi maandiko mengine jinsi mfalme alivyowajibu watu wale baada ya kumrudia siku ya tatu. Kutokana na mapatano yao ya kuja kumsikiliza mfalme ameamua nini kuhusu ombi lao.

Rejea: Basi Yeroboamu na watu wote wakamjia Rehoboamu siku ya tatu, kama mfalme alivyoamuru, akisema, Mnirudie siku ya tatu. Mfalme akawajibu kwa ukali; mfalme Rehoboamu akaliacha shauri la wazee, akasema nao kwa shauri la vijana, akinena, Baba yangu aliwafanyia kongwa zito, nami nitawaongezea; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa nge. 2 NYA. 10:12‭-‬14 SUV.

Naomba uelewe hapa, vyema kama haupo tayari kufuata ushauri mwema usiende kuutafuta. Bora ukaenda moja kwa moja kwa watu ambao unajua watakupa maneno ya kukuongezea hamasa ya kutenda baya ulilokusudia kulitenda.

Nakueleza haya kwa sababu ya wengi wetu tumekuwa na tabia hii ya kusumbua watu ambao unajua kabisa haupo tayari kufuata kile ambacho watakuelekeza.

Usifungiwe mipaka pia, kama unaona jambo linakupa utata na hujui ufanye nini,na haupo tayari kufuata ushauri wa wengine. Nenda mbele za Mungu usikie anakupa maelekezo gani ya kuchukua hatua, hapo lazima uombe mapenzi ya Mungu.

Naamini umepata kitu cha kufanyia kazi katika suala zima la kuomba ushauri kwa wengine. Hicho ulichojifunza kifanyie kazi, utafanikiwa katika mambo yako.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Ndugu yako katika Kristo

Chapeo Ya Wokovu
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.