Mungu wetu anapenda mtu msafi mbele zake, ndio maana unapaswa kujitakasa kwanza kabla hujafanya mambo mengine zaidi kwake.
Kujitakasa kwako kunamfanya Mungu akuhudumie vizuri, kile unakihitaji kutoka kwake.
Wengi wetu tumelipuuzia hili sana, tumeona kawaida na ukawaida huu umetuponza mambo mengi sana.
Kujitakasa mbele za Mungu ni mhimu sana, jenga utaratibu huu katika maombi yako kila siku.
Kujitakasa kunakuja baada ya kuomba toba mbele za Mungu, kutubu pia inapaswa kuwa desturi ya mkristo mwenda mbinguni. Maana yapo mambo tunajikwaa pasipo kujua, yapo mambo tunakoseshwa na macho ya nyama, yapo mawazo mabaya hutujia, yapo mazungumzo mabaya hushiriki pasipo kuelewa haraka.
Ukielewa haya moyo wako utajaa unyenyekevu na toba mbele za MUNGU, toba ile inakupeleka hatua nyingine ya kujitakasa kwa damu ya Yesu Kristo aliye hai.
Ninapozungumza kujitakasa, sizungumzi kwenda kuoga ziwani/bwawani, au kuoga kwa sabuni nzuri. Kujitakasa ninayoizungumza hapa ni kwa kutumia damu ya Yesu.
Damu ya Yesu Kristo inatakasa kila uchafu ulio ndani ya mwa mtu, ikiwa mtu yule ataenda mbele za Mungu kwa kumaanisha kile anaomba.
Mfalme Daudi alilijua hili mapema sana, alijua pasipo kujitakasa haiwezekani kusogelea saduku la Bwana.
Tunaona walawi wakipewa maagizo ya kujitakasa kwanza kabla ya kutekeleza wajibu wao waliopewa na Mungu, wa kulibeba na kulilinda sanduku la Bwana.
Kumbe Mungu anaweza kukuchagua umtumikie, ila akataka uvue utu wa kale kwanza kwa kujitakasa mbele zake.
Haya tunayaona kwenye mstari huu;
Akawaambia, Ninyi ni vichwa vya mbari za baba za Walawi; jitakaseni, ninyi na ndugu zenu, ili mlipandishe sanduku la Bwana, Mungu wa Israeli, mpaka mahali pale nilipoliwekea tayari. 1Nya 15 :12.
Umeona jinsi gani Daudi alivyotoa maagizo ya kujitakasa kwanza, ndipo waweze kulishika sanduku la Mungu.
Kumbe kabla ya kutoa huduma madhabahuni, tunapaswa kujitakasa kwanza ndipo tuweze kuhudumia wengine.
Zingatia sana hili katika maisha yako ya WOKOVU, utaona nguvu za Mungu zikiambatana nawe kila wakati.
Mungu akusaidie uelewe zaidi umhimu wa kujitakasa kwanza kabla ya huduma, au kabla ya kutumika mbele za MUNGU kuwahudumia watu wake.
Samson Ernest.
+255759808081.