Mungu kukaa mbali nasi, mara nyingi husababishwa na sisi wenyewe, yale maovu yetu tunayatenda husababisha Mungu awe mbali nasi. Kule kuchanganya miungu mingine na yeye, huondoa kabisa uwepo wake.

Kule kuabudu sanamu za wakuu wetu waliopita, huleta hasira Mbele za Mungu na kuondoa kabisa uwepo wake kwetu. Tunaanza kujikuta tunakaukiwa zaidi kihuduma kutokana na kosa kubwa tulilomtenda Mungu wetu.

Tunao uwezo wa kumfanya Mungu aongoze hatua zetu au tunaweza kumfanya Mungu akae mbali kabisa na Mambo yetu. Unaweza kujikuta unatafuta msaada wa Mungu, ila Mungu akawa mbali na wewe.

Tunafanyaje ili Mungu awe kiongozi wa maisha yetu? Lazima tukubali kuyapa mgongo/kisogo mambo yote mabaya yanayomkosea Mungu wetu.

Rejea: Basi sasa wayaondoe mambo yao ya kikahaba, na mizoga ya wafalme wao, yawe mbali nami, nami nitakaa kati yao milele. EZE. 43:9 SUV.

Ukitaka kurejesha uhusiano wako na Mungu, achana na mambo mabaya yanayomchukiza Mungu. Unaweza kufikiri Mungu yupo pamoja na wewe, kumbe ameshakuacha siku nyingi.

Ondoa sanamu za kifalme moyoni mwako, mruhusu Yesu Kristo atawale moyo wako. Utaona baraka za Mungu zikianza kutenda kazi katika maisha yako.

Chagua njia sahihi kwako, njia inayokuwezesha kujenga uhusiano mzuri na Mungu wako. Elewa kwamba, kama unasema umeokoka alafu unaabudu sanamu, fahamu huo ni uongo. Unapaswa kumrudia Mungu wako.

Kama unaabudu miungu ya mababu zako huku unasema wewe umeokoka, bado hujajua maana ya wokovu. Mkristo yeyote hawezi kuchanganya miungu ya mababu zake na Mungu wa kweli.

Tumeshaona kufanya hivyo ni kuondoa ushirika mzuri na Mungu wetu, unapoamua kulikiri jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai. Unapaswa kuachana na mambo mengine mabaya, ambayo yatakuondolea uwepo wa Mungu.

Tubu dhambi zako zote leo ili Roho Mtakatifu aingie ndani yako, bila kufanya hivyo utakuwa unajidanganya. Vyema kujipambanua mapema, usije ukafika mahali ukaona maisha yako yanaenda hovyo.

Mungu akubariki sana.