Kama kuna eneo tunahitaji Mungu atusaidie sana ni hili la kutofuata maelekezo tunayopewa.

Wengi watu tunafeli kwa sababu ya kutozingatia maelekezo tunayopewa.

Wengi wetu tunashindwa kusogea hatua moja kwenda nyingine kwa kutozingatia maelekezo tunayopewa.

Wengi wetu tunashindwa kusogea hatua moja ya kiroho kwenda hatua nyingine kutokana na kutozingatia maelekezo.

Kukaa kwetu kwenye nafasi fulani bila kusogea hatua nyingine mbele wakati mwingine ni kushindwa kwetu kuzingatia maelekezo.

Hili tunaliona kwa Rahabu akiwapa maelekezo wale wapelelezi walioenda kuipeleleza nchi yao ya ahadi.

Rejea: Akawaambia, Enendeni zenu mlimani, wale wanaowafuatia wasije wakawapata; mkajifiche huko siku tatu hata wao wanaowafuatia watakaporudi; kisha enendeni zenu. YOS. 2:16 SUV.

Hawakupuuza maneno haya ya Rahabu aliyowapa hawa wapelelezi waliowaficha juu ya dari.

Hawakusema huyo mwanamke naye anasema nini hichi, atakuwa haelewi tu  sisi ni taifa kubwa linalotumiwa na Mungu.

Wapelelezi hawa walimsikiliza Rahabu, na hili tunalithibitisha kupitia maandiko haya.

Rejea: Watu hao wakaenda, wakafika mlimani, wakakaa huko siku tatu, hata wale waliowafuatia walipokuwa wamerudi; na wale waliowafuatia wakawafuatia katika njia ile yote, lakini hawakuwaona. YOS. 2:22 SUV.

Yapo mambo ambayo tunakutana nayo na yanahitaji tuzingatie sana maelekezo tunayopewa.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com